FAO na wadau wazisaidia nchi kukabiliana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba

3 Oktoba 2019

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO kwa kushirikiana na wadau linaongeza juhudi za kuzisaidia nchi kupambana na tishio kubwa la ugonjwa wa mnyauko wa migomba unaoathiri uzalishaji wa ndizi kwa kuzindua mradi maalum.

Mradi huo wa FAO uliozinduliwa leo ni mradi wa dharura ulio chini ya mpango wa ushirikiano wa kiufundi wa kuzisaidia nchi za Amerika ya Kusini na visiwa vya Caribbea kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa mnyauko wa migomba  maarufu kama Fusarium wilt, ugonjwa wa  fangasi wa mimea ambao unaweza kuangamiza zao la ndizi ambalo linategemewa na mamilioni ya watu kwa ajili ya chakula na kuishi.

 

Shirika la FAO linasema ugonjwa huo ulioshika kasi hivi karibuni unaathiri uzalishaji wa aina nyingi za ndizi ikiwemo aina ya kinguruwe au Cavendish zinazopendwa katika masoko duniani kote  ugonjwa huo ambao pia hujulikana kama TR4 unaathiri zaidi mizizi na mashina mgomba, na ingawa hauna athari zozote kwa binadamu unaweza kusababisha hasara ya asilimia 100 na kuwa ni zahma kubwa kwa nchi na jamii ambazo uzalishaji wan dizi ndio chanzio kikubwa cha chakula, kipato cha familia na pato la usafirishaji nje bidhaa.

Kwa sasa FAO inasema ekari 175 za mashamba ya ndizi yamewekwa chini ya karantini  nchini Colombia  karibu na Equador nchi ambayo ni msafirishaji mkubwa wan dizi duniani  ikifuatiwa na Colombia, Costa Rica na Guatemala , na endapo ugonjwa huo utaruhusiwa kusambaa FAO imeonya kwamba utaleta athari kubwa kwa wakulima, familia zao na ukanda mzima .

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud