Ukame wawalazimu Wasomali zaidi kufungasha virago kuingia Ethiopia: UNHCR

3 Oktoba 2019

Hali mbaya ya ukame na usalama nchini Somalia imewalazimu maelfu wa watu kuendelea kufungasha virago tena na kukimbia nchi jirani ya Ethiopia kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR. 

Kwenye kambi ya wakimbizi nchini Ethiopia, Bwarako Abdi ni miongoni mwa maelfu ya Wasomali waliolazimika kukimbia mara ya pili. Mara ya kwanza ilikuwa 2011 na miezi miwili iliyopia wakafunga virago tena,sababu kubwa ni ukame na hali tete ya usalama

(SAUTI YA BWARAKO ABDI-1)

“Kuna ukame na vita visivyokwisha “

Akiwa amekimbia na watoto wake takriban saba anasema

(SAUTI YA BWARAKO ABDI -2)

“Katika ukame wa kwanza 2011, tulipoteza ng’ombe wetu wote na mbuzi karibu nusu niliondoka kwa sababu ya watoto wangu , nataka watoto wangu wafanikiwe na kuwa na mustakabali bora . Kuishi shambani wakati kuna ukame siku zote ni vigumu , nimelea watoto wangu katika mazingira magumu . Sitokubali asilani watoto wangu wachukuliwe na wapiganaji”

Ethiopia imeshapokea wakimbizi 5000 wa Kisomali mwaka huu, takribani mara nne ya idadi ya waliowapokea mwaka 2018.

Wakimbizi hao wanawasili kila uchao. Muhammad Harfoush ni afisawa ulinzi wa UNHCR

(SAUTI YA MUHAMMAD HARFOUSH)

“Wakimbizi wapya hawajawahi kusita kuingia Ethiopia, hivyo kila mwaka tunapata watu wapya wanaokuja wakieleza changamoto za kufanana kuhusu ukame, kutokuwa na usalama, upungufu wa chakula na maji, na wanaowasili kila siku wanahifadhiwa katika kituo cha mapokezi, na kisha kuhamishiwa makambini kulingana na uwepo wa malazi, hiyo ndio changamoto kubwa tuliyonayo tunajaribu kuishughulikia”.

Kutokana na mzunguko wa ukame wafugaji na wakulima wanhaha kukabiliana na hali.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud