Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yataka kasi ya uhamishaji wa wakimbizi wakati kukishuhudiwa mlundikano Ugiriki

Familia kutoka Syria ambao wamewasili huko Lesvos, Ugiriki wakisaka hifadhi katika kituo cha mapokezi cha Moria. Septemba 23, 2019.
© UNHCR/Gordon Welters
Familia kutoka Syria ambao wamewasili huko Lesvos, Ugiriki wakisaka hifadhi katika kituo cha mapokezi cha Moria. Septemba 23, 2019.

UNHCR yataka kasi ya uhamishaji wa wakimbizi wakati kukishuhudiwa mlundikano Ugiriki

Wahamiaji na Wakimbizi

Ongezeko la idadi ya wakimbizi wanaowasili katika vituo vya mapokezi nchini Ugiriki huenda ikafanya hali ya sasa ya mlundikano kuwa mbaya zaidi, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Wakati wito ukitolewa wa kuhamisha waomba hifadhi hadi maeneo ya katikati ya Athens, mji mkuu wa Ugiriki, UNHCR imeripoti kwamba idadi ya watu wanaowasili kwa njia ya baharí mwezi uliopita wa Septemba ni zaidi ya 10,000,  hii ikiwa ni idadi ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 2016.

Hatua hii ni kufuatia tukio la Jumapili katika nyumba ya kituo cha mapokezi cha Moria huko Lesvos ambako mwanamke mmoja alifariki na tukio hilo kuzua maandamano makali.

Kwa mujibu wa UNHCR, kuna zaidi ya watoto 4,400 katika visiwa hivyo ambao wamesafiri bila walezi kati ya watu 30,000 wanaosaka hifadhi.

Watoto 500 kati ya idadi hiyo wanahifadhiwa pamoja na watu ambao sio jamaa zao katika vyandarua huku shirika hilo ikitaja hali inayoshuhudiwa huko Lesvos, Samos na Kos kama mbaya.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, msemaji wa UNHCR Liz Throssell ameelezea haja ya hatua za haraka kutoka mamlaka za Ugiriki kuharakisha uhamishwaji wa waomba hifadhi 5,000 ambao tayari wanaruhusa ya kueomba hifadhi katika maeneo ya bara.

Huko Lesvos katika kituo cha Moria kina watu 12,600 ambayo ni mara tano zaidi ya uwezo ambapo huku katika makazi yasiyo rasmi takriban watu mia moja wanatumia choo kimoja.

Huko Samos, kituo cha Vathy kinahifadhi watu 5,500 ikiwa ni mara nane zaidi ya uwezo na Kos watu 3,000 wanaishi katika eneo la watu 700.

UNHCR imesema wengi wa wale wanaosaka hifadhi ni kutoka Afghanistan na Syria pamoja na Iraq na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wakati huo huo UNHCR imekaribisha tangazo la serikali ya Ugiriki ya kuondoa shinikizo visiwani na kulinda watoto wanaosafiri bila walezi.

Kwa mujibu wa UNHCR, Ugiriki imepokea watu 45,600 kati ya 77,400 ambao wanavuka baharí ya Mediterranea mwaka huu ikilinganishwa na idadi ya pamoja ya Uhispania, Italia, Malta na Cyprus.

Idadi ya vifo kutokana na ajali za baharí ya Mediterrabea imefika 1000 kwa mwaka wa 6 mfululizo

Wakati huo huo kwa mwezi wa sita mfululizo, watu 1,000 wameripotiwa kuzama wakati wa safari kupitia baharí ya Mediterranea limesema shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji duniani IOM, leo Jumanne.

Likitolea mfano wa ongezeko la ajali za meli katika njia za uhamiaji barani Ulaya ambazo zimesababisha ongezeko la idadi ya watu waliopoteza maisha, IOM imetaja tukio la mweisho wa wiki jana katika pwani ya Morocco ambapo takriban watu 40 wanashukiwa kuzama maji.

Katika kipindi cha miaka 6, takriban watu 15,000 wanaume, wanawake na watoto wamepoteza maisha yao wakijaribu kufikia Ulaya kwa kutumia boti hali ambayo IOM imetaja kama “mauaji baharini”

Kwa mujibu wa IOM safari hatarishi zaidi ni ile ya Mediterranea kati kutoka Afrika Kaskazini hadi Italia ambapo wahamiaji 659 au wakimbizi wamepoteza maisha yao mwaka huu.

Takriban watu wengine 270 wamefariki wakati wakijaribu kufika Uhispania kutoka Afrika Kaskazini, huku waathirika 66 wameripotiwa katika njia ya mashariki mwa bahari ya Mediterranea kupakana na Uturuki, Syria na Ugiriki.