Maisha ya mzee yasalia mashakani, Uganda

1 Oktoba 2019

Leo Oktoba Mosi ni siku ya wazee duniani ambapo mwaka huu kauli mbiu ni “safari ya kuzeeka kwa usawa” kwa kutambua kwamba malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yatafikiwa pale tu watu wa umri wote wamejumuishwa.

Lakini hali mashinani ikoje? Mwandishi wetu John Kibeog kutoka Uganda amezungmuza na Wazee Peter Semiga na Nathan Kitwe Isingoma ambaye pia ni Spika wa Halmashauri ya wilaya ya Hoima kufahamu hali ya wazee katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Mzee Peter anaanza kwa kujitambulisha kisha anaeleza kuhusu maisha yake ya uzee katika jamii, “Semiga Peter ndilo jina langu, kusema kweli naishi maisha magumu. Watu ambao ninaishi nao hawanitambui kama mzee.  Kwa mfano kama nikienda kupata matibabu wananiona kama mtu ambaye hafai kupata matibabu au kupata huduma zozote. Vijana huenda kwa kusukuma, badala ya kuwa katika foleni unajikuta umeshasukumwa nje, hiyo inanifanya vibaya hata nasikia kichwa kinazunguka.”

Hapo Mzee Seminga anatoa ushauri kwa serikali,“naiomba serikali ya Uganda itilie mkazo tukienda kupata huduma  tupatiwe foleni ya wazee bila kupata tabu yoyote.”

Naye Nathan Kitwe Isengoma anasema, “kwakweli hali ya wazee hapa nchini Uganda siyo nzuri.  Yaani kuna vitu vingi kabisa ambavyo vinawasumbua wazee.  Wapate nguo za kuvaa, vyakula na kadhalika. Kuna wilaya nyingine ambazo kulikuwa na mradi wa majaribio walikuwa wanapata elfu 25 kwa mwezi mzima, hapa Hoima hatujapata kitu.  Hata hizo elfu 25 siyo pesa za kutosha, unaweza kupata kilo tatu nne hivi ya  sukari na  chumvi halafu zinaisha.

Je, Isengoma anapendekeza nini?, “Serikali ingewapangia wazee sehemu fulani za kukaa kama ilivyo katika nchini kwa mfano huko China ambako  wazee wanakusanywa sehemu moja kupata mahitaji kama nguo na burudani.”

Aidha Mzee Isengoma anawakumbusha viongozi kama wabunge kuwa kesho nao watakuwa wazee kwa hivyo wanapokuwa wanatunga sera, wawatetee wazee ili kupata usaaidizi badala ya jamii kuwaona kama watu waliopitwa na wakati.

 

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter