Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikao cha kwanza cha kamati ya kikatiba Syria kufanyika Oktoba 30

Geir Pedersen,mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria akilieleza Baraza la Usalama kuhusu hali ya Syria.
Kim Haughton/Picha ya UN
Geir Pedersen,mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria akilieleza Baraza la Usalama kuhusu hali ya Syria.

Kikao cha kwanza cha kamati ya kikatiba Syria kufanyika Oktoba 30

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha wazi kuhusu Syria ajenda kuu ikiwa ni hali ya kisiasa nchini humo wakati huu ambapo tayari kamati jumuisha ya kikatiba imeudwa kufuatia makubaliano kati ya serikali na kamati ya usuluhishi ya Syria.

Akihutubia washiriki, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Geir O. Pedersen amesema  tarehe 30 mwezi ujao wa Oktoba ataitisha kikao cha kamati hiyo yenye wajumbe 150 wanawakena wanaume, ikiratibiwa na Umoja wa Mataifa.

“Naamini hii itakuwa ishara ya matumaini kwa wananchi wa Syria ambao wamekumbwa na machungu kwa muda mrefu na kikao kitafanyika kufuatia makubaliano kati ya serikali ya Syria, kamisheni ya usuluhishi ya Syria kuhusu wateule wa kamati hiyo, hadidu za rejea na kanuni za msingi za kuongoza kazi zao,” amesema Perdesen.

Umuhimu wa makubaliano

Amewajulisha wajumbe watambue umuhimu wa hatua hiyo kwa kuzingatia ni makubaliano ya kwanza kabisa ya kisiasa kati ya serikali na upinzani nchini Syria katika kuanza kutekeleza azimio namba 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kupanga ratiba na mchakato wa mapitio ya katiba.

Misingi mikuu ya makubaliano  hayo ni kuheshimu katiba ya Umoja wa Mataifa, maazimio ya Baraza la Usalama, uhuru, mamlaka na umoja wa Syria na mchakato ambao unaongozwa na kumilikiwa na wasyria wenyewe.

Makubaliano haya yanaleta wawakilishi kutoka pande kinzani kuketi meza moja na kufanya mashauriano na wakati huo huo pia wajumbe wa asasi za kiraia,” amesema mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria.

Je majina yanafahamika?

Kwa mujibu wa Perdesen, majina ya wajumbe hao 150 yatangazwa na Umoja wa Mataifa baada ya wateule hao kuthibitisha rasmi ushiriki wao. “Hata hivyo hebu nizungumze kuhusu wateule hao. Kando ya wateule kutoka serikalini, upinzani, theluthi moja wanatoka asasi za kiraia za dini, makabila na maeneo tofauti wakiwemo wataalamu. Wengine wanaishi Syria, wengine wanaishi nje ya Syria,” amesema Bwana Pedersen.

Asilimia 30 ya wajumbe 150 ni wanawake

Amesema kuwa wanajivunia kuwa nusu ya wateule kutoka asasi za kiraia ni wanawake na kwamba asilimia 30 ya wajumbe wote 150 pia ni wanawake. “Mchakato wowote bora na endelevu wa amani ni lazima uwe na wanawake ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya wat una ambao katika kipindi chote cha vita wamekuwa na dhima muhimu zaidi kwenye jamii zao,” amesisitiza Bwana Pedersen.

Hata hivyo Bwana Pedersen amekumbusha kuwa kutumia vyema fursa ya sasa haitakuwa jambo rahisi kwa kuzingatia kuwa bado Syria imeghubikwa na mapigaon na ugaidi huku majeshi matano ya kimataifa yakiwa nchini humo, machungu na ukatili vikiendelea kukumba wasyria, imani nayo ikiwa imetoweka.

“Kamati hii ya kikatiba itakuwa na umuhimu iwapo itakuwa ni fursa ya kuepusha wasyria na janga la sasa na kuwa na Syria mpya na hatimaye irejeshe imani miongoni mwa wasyria na kati ya Syria na jamii ya kimataifa,” amesema Bwana Pedersen.aa