Kamata kamata kufuatia maandamano Misri inatutia hofu kubwa:Bachelet

27 Septemba 2019

Kamishina mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet leo Ijumaa ameelezea wasiwasi mkubwa alionao kuhusu taarifa za kutokuwepo mchakato wowote kufuatia idadi kubwa ya kamata kamata ya watu ikihusishwa na maandamano nchini Misri, na kuutaka uongozi wa Misri kuheshimu haki ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani kwa kutekeleza kanuni na viwango vya kimataifa.

Kwa mujibu wa mashirika ya asasi za kiraia zaidi ya watu 200 wakiwemo wanasheria, watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati wa kisiasa, maprofesa na waandishi wa Habari waliswekwa mahabusu wakati na baada ya maandamano yaliyofanyika katika miji mbalimbali nchini Misri tarehe 20-21 Septemba.

Ofisi ya Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu amepokea taarifa kwamba baadhi ya wale waliokuwa wakishikiliwa wameachiliwa. Taarifa pia zinaonyesha kwamba watu walioshikiliwa walinyimwa dhamana na uwakilishi wa kisheria wakati walipipanda kizimbani na wengine wanadaiwa kuhukumiwa kwa makosa makubwa zaidi.

Mashitaka hayo yanajumuisha kusaidia makundi ya kigaidi ili kufikia malengo yao , kusambaza taarifa za uongo, kushiriki katika maandamano yasiyo idhinishwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Bi. Bachelet ameongeza kuwa “Naikumbusha serikali ya Misri kwamba chini ya sheria za kimataifa  watu wana haki ya kuandamana kwa amani” Pia wana haki ya kuelezea maoni yao ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii. Hawakustaili kuwekwa rumande , ukiachilia mbali makossa makubwa waliyofunguliwa mashitaka kwa kutekeleza haki zao za msingi.”

Ametoa wito kwa serikali kubadili mtazamo dhidi ya maandamano yoyote yatakayofanyika siku za usoni, na wale wote walioshikiliwa kwa kutekeleza haki zao za msingi waachaliwe mara moja.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud