Vifaa muhimu ili kudhibiti milipuko ya kipindupindu vimewasili nchini Sudan-WHO

26 Septemba 2019

Shehena ya tani 36 za dawa na vifaa tiba dhidi ya kipindupindu vimewasili mjini Khartoum, Sudan na vinaandaliwa kusambazwa ikiwa ni shemu ya msaada wa shirika la afya duniani WHO kwa Sudan kupambana na mlipuko wa Kipindupindu.

Taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa WHO imeeleza kuwa shehena hiyo imebeba, pamoja na mambo mengine, vifaa vya dharura vya kupima ugonjwa RDTs vipatavyo 5000 kwa ajili ya kuwachunguza wagonjwa waliko katika vituo vya afya na katika maeneo yaliyoko hatarini.

Shehena hiyo pia imebeba dawa zinazoweza kuwatibu watu 2500 walioko katika hali mbaya baada ya kupoteza maji mwilini. Mzigo huo utasambazwa katika vituo vya matibabu kwenye majimbo ya Blue Nile na Sinnar ambako visa vya Kipindupindu vimeripotiwa, pia katika maeneo ya majimbo jirani yaliyoko hatarini kama vile White Nile, Kassala, Gedaref na Khartoum.

Mwakilishi wa WHO nchini Sudan Dkt Naeema Al Gasseerm amesema, “tunakimbizana na muda pamoja na wizara ya afya ya Sudan, mamlaka za serikali na wadau wengine kudhibiti mlipuko na kuzuia vifo zaidi.”

Kwa mujibu wa WHO, hadi kufikia juzi tarehe 24 Sptemba 2019, jumla ya visa 184 vimeripotiwa, vikiwemo visa 128 katika jimbo la Blue Nile na visa 56 katika jimbo la Sinnar. Wizara ya afya ya Sudan imeripoti vifo nane vinavyohusaiana na kipindupindu ambapo visa 6 ni katika jimbo la Blue Nile na vifo viwili kutoka jimbo la Sinnar.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud