Tunaomba jamii ya kimataifa kwenda nasi bega kwa bega kutatua majanga CAR - rais Touadera

25 Septemba 2019

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Faustin Archange Touadera hii leo Jumatano ametoa wito wa ushirikiano wa kimataifa, tofauti, unaoeleweka, na ulio na utaratibu katika kukabiliana na janga linalokabili nchi yake, akielezea msaada wa serikali kuendelea kusaidia raia wake kuibuka kutoka hali ya sasa. 

Akihutubia mjadala wa mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74, Rais Touadera amesema, “hali nchini mwangu bado ni dhaifu licha ya hatua zilizopigwa. Makundi yaliyojihami yanaendelea kupokea silaha na risasi kwa njia zisizo halali. Wanatekeleza ukiukaji wa jumla na wa mara kwa mara wa haki za kimataifa za kibinadamu na sheria za kibinadamu.”

Rais huyo amekaribisha kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama namba 2488 la mwaka 2019 kuhusu kulegeza vikwazo dhidi ya silaha na kutoa wito liondolewe kabisa.

Rais Touadera amesema, “ili kuibuka kutoka mzozo ambao umetikisa nchi yangu na kwa kuzingatia kaulimbiu ya mkutano huu, natoa wito wa hatua za pamoja, zinazoeleweka na zilizopangwa za kimataifa. Nina matumani kwamba jamii ya kimataifa itasalia bega kwa bega na watu na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na itaendelea kuwasaidia katika kutoka kwa hali ya sasa.”

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa  wa kulinda amani nchini CAR, MINUSCA ulianzishwa mwaka 2014 ukiwa na kipaumbele cha kulinda raia. 

Jukumu lingine la ujumbe huo ni kuunga mkono mchakato wa mabadiliko, kwa kutoa msaada wa kibinadamu, kuimarisha na kulinda haki za binadamu, kusaidia vyombo vya haki za usimamizi wa sheria, upokonyaji silaha, kuvunja makundi ya yaliyojihami, kuwajumuisha tena kwenye jamii na kuwarejesha makwao.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud