Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita bado ni chanzo kikubwa ya ukiukwaji wa haki za mtoto:Guterres

Watoto darasani Sakassou, Côte d'Ivoire.(8 Julai 2019) Chris Mburu anapigania elimu nchini mwake Kenya akiamini elimu ndiyo ufunguo wa kila kitu maishani
© UNICEF/Frank Dejo
Watoto darasani Sakassou, Côte d'Ivoire.(8 Julai 2019) Chris Mburu anapigania elimu nchini mwake Kenya akiamini elimu ndiyo ufunguo wa kila kitu maishani

Vita bado ni chanzo kikubwa ya ukiukwaji wa haki za mtoto:Guterres

Haki za binadamu

Tangu kupitishwa kwa mkataba wa haki za mtoto miaka 30 iliyopita pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kote duniani bado vita imesalia kuwa chanzo kikubwa cha ukiukwaji wa haki za mtoto na bado kuna nchi hazijaridhia mkataba huoamesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. 

Katibu Mkuu akizungumza katika hafla leo jijini New York Marekani katika mjadala Mkuu wa Baraza Kuu , amesema “mkataba huo (CRC) unatambua kwamba mtoto ana haki ya kulindwa na kuwa na uhakika wa usalama wao majumbani, wanakoishi na vijijini kwao, wana haki ya kutoa maoni yao na kusikilizwa na mkataba huu ni moja ya mikataba ya Umoja wa Mataifa iliyoridhiwa na nchi nyingi sana katika historia. Lakini bado kuna baadhi ya nchi wanachama ambao bado hawajafanya hivyo na matarajio ni kufikia siku ambayo wajumbe wote wataunga mkono mkataba huu.

Hata hivyo amesema, “kuchukua au kutochukua hatua kwa serikali kuna athari kubwa kwa watoto kuliko kundi lingine lolote katika jamii, watoto wako katika hatari ya umasikini, njaa, afya duni na maisha wasiyostahili. Lakini kwa juhudi zilizofanyika haki sasa imedhihirika kwa mamilioni ya watoto. Lakini hatuwezi kumudu kubweteka , tunahitaji kuimarisha juhudi zetu kuhakikisha kwamba watoto wote wako salama, wana afya na wanaweza kutimiza ndoto zao.”

Ameongeza kuwa uwezo wa mtoto unaweza kudumazwa kutokana na lishe duni kabla ya umri wa miaka miwili ambalo hilo ni tatizo kubwa kwa mamilioni ya watoto husan walio kwani maisha ya mtoto huanza kuandaliwa wakati anaanza shule.

Mafanikio ya miaka 30 ya mkataba wa haki za mtoto

Amesema kwa kiasi kikubwa mkataba wa haki za mtoto kuchagiza hatua kwas asa watoto wengi zaidi kuliko wakati mwingine wowote wanapata ulinzi na msaada wanaouhitaji . Katika miaka 30 iliyopita vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka 5 vimepungua kwa nusu na pia idadi ya watoto wenye utapiamlo.Katika sehemu nnyingi serikali na asasi za kiraia wanashirikiana kutoa msaada kwa watoto walio katika maeneo ya vita kukomesha ndoa za utotoni na kuwapa watoto hao na vijana sauti katika maamuzi ambayo yanawahusu.

Guterres amesema “miaka 30 iliyopita mataifa yaliungana pamoja kutoa ahadi kwa watoto wa dunia hii. Waliahidi sio tu kutekeleza haki zao lakini pia kuzidumisha na kuwajibika nazo. Na mkataba wa haki za mtoto (CRC) ulikuwa ni mafanikio ya kihistoria. Kwa mara ya kwanza serikali zilitambua kwamba watoto wana haki sawa kama watu wazima, pamoja na haki zingine za ziada kama watu walio tegemezi.”

Yaliyomo katika CRC

Mkataba wa CRC unatambua haki za mtoto za afya, dawa na lishe. Haki ya kupata maji safi na usafi, haki ya watoo kupata elimu , kukaa darasani ikiwemo watoto wenye ulemavu na walio katika maeneo ya vita.

Hatua zaidi bado zahitajika

Guterres amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana  bado juhudiu zaidi zinahitajika kwani mamilioni ya watoto kote duniani badi wanakabiliwa na njaa, maradhu au hatari na wengine wanateseka kwa sababu ya dini zao , kabila lao nau ulemavu wao.

Watoto walio katika vita wako katika hatari ya ukatili wa hali ya juu wa kingono ambao huwasababishia majerahha ya muda mrefu ya kisaikolojia. Pia Watoto ambao ni waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu umeongezeka Zaidi ya mara mbili kutoka mwaka 2004 hadi 2016 na wengi wanasafirishwa kwa ajili ya utumwa wa ngono, wanashinikizwa kufanya kazi na kuingizwa vitani kama askari Watoto Katibu Mkuu amesisitiza ni lazima tubadili mwenendo huu kwani ni mwenendo usio kubalika. Na wasichana ndio walio katika hatari zaidi ya ndoa za utotoni , ukatili wa ngono na ukatili mwingine,ndio wengi wanaokosa fursa za kusoma na kukosa chakula na pia kubeba mzigo wa kazi za nyumbani zisizo na malipo.

Changamoto zilizopo kwa watoto

Umoja wa Mataigfa unasema changamoto mpya ni pamoja na ongezeko la pengo la usawa na teknolojia ya dijitali ambavyo vinawaweka watoto katika hatari kubwa. Watoto wa leo amesema pia watakabiliwa na mtihani mkubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi endapo kizazi hiki kitashindwa kuchukua hatua sasa kuzuia hilo. Familia nyingi zinahama sasa kuliko wakati mwingine wowote na Watoto wa wahamiaji ndio walio hatarini zaidi duniani kote.

Naye binti mdogo kutoka Ghana aliyeiwakilisha nchi yake na watoto wote wa Afrika amesisitiza, “ndio tumepiga hatua lakini bado kuna mengi ya kufanya kwa watoto wanaoishi katika umasikini na kutelekezwa, kwa watoto wanaoishi katika vita, ukimbizi na jamii za wahamiaji”

Guterres amesema vita ni moja ya tishio kubwa kwa utimizaji wa haki za mtoto na vinaongeza ukubwa na vitisho vingine na amani ndio njia bora zaidi ya kuwalinda watoto.

Hivyo amewataka nchi zote wanachama wakati huu wa kuadhimisha miaka 30 ya mkataba huo wa kihistoria kurejelea ahadi zao za kuwapa kipaumbele cha kwanza watoto, “nawataka nyote kutia saini ombi la kimataifa la kuimarisha ahadi zenu kuhusu mkataba wa haki za mtoto. Kwa pamoja hebu twende kwa kasi ya kufikia yaliyojiri kwa miaka 30 iliyopita na zaidi kwa ahadi mpya , kwa kila mtoto , kwa kila haki.”