Wajibu wa kutekeleza SDGs ni wa ulimwengu mzima-Dkt Philip Mpango

24 Septemba 2019

Waziri wa fedha na mipango wa Tanzania, Dkt Philip Mpango ametoa wito wa jumuiya nzima ya kimataifa kuwajibika kwa pamoja ili kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu SDGs kwani ili lengo moja litimie katika nchi moja, pia linahitaji uwajibikaji wa nchi nyingine.

Dkt Mpango anaeleza hayo mjini New York Marekani alipozungumza na UN News idhaa ya kiswahili kandoni mwa jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa HLPF linalotathimini utekelezaji wa malengo hayo kwa nchi wanachama 50 waliojitolea kufanyiwa tathimini ikiwemo Tanzania.

(Sauti ya Dkt Mpango)

“Ni muhimu jumuiya ya kimataifa itambue kwamba wajibu wa kutekeleza haya malengo ni wa ulimwengu mzima, na hususani baadhi ya nchi ambazo zinaonekana zinavuta miguu hususani katika suala la kupunguza hewa ya ukaa ambayo inatuathiri wote. Wafunguke, wasipofunguka ulimwengu wetu huu unazidi kuharibika. Kuna nchi mimi nimekenda hata kupumua ni shida. Yaani unaona kama hewa yote imejaa moshi. Kwa hivyo ni vizuri kila nchi ione dhamana kwamba binadamu tunao wajibu wa kutunza hii dunia ili itutunze,”  anasema Dkt Mpango.

Miongoni mwa mifano mingine, Dkt Mpango, anagusia utoroshaji fedha ambao unategemea intelijensia za kimataifa, kisha anaeleza jinsi Tanzania inavyopiga hatua katika kutekeleza SDGs, akisema, kando ya ujenzi wa viwanda na uboreshaji wa sekta ya afya, Tanzania kila mwezi inatenga bilioni 23 za Tanzania sawa na takribani dola milioni 10 kila mwezi  kulipia elimu ya msingi na kisha anaeleza kuhusu ukuaji wa uchumi anasema,

(Sauti ya Dkt Mpango)

“Tanzania ni moja kati ya  nchi 10 ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.  Kwa mwaka 2017 uchumi w anchi yetu umekuwa kwa asilimia 7, tunazidiwa kidogo na Ethiopia ambayo uchumi wake unakua kwa asilimia 8. Lakini hiyo haitoshi maana unaweza ukakua kwa namba, lakini ukienda kwenye takwimu za kasi ya kupungua kwa umaskini,  kutoka mwaka 2011/12, watanzania waliokuwa wanaishi chini ya kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi, walikuwa asilimia 28.2, lakini mwaka 2017/18 tumefanya tena tathmini ambayo inaonesha kiwango cha umaskini kimeshuka na kuwa asilimia 26.4. Si haba, tungependa tupate zaidi lakini takwimu halisi zinaonesha hivyo. Kwa hiyo tunapiga hatua.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter