Greta Thunberg ahoji uthubutu wa viongozi kusalia na maneno huku watu wakipoteza maisha

Mtizamo wa Baraza Kuu wakati wa ufunguzi wa kongamano la hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi mwaka 2019. (Septemba 23, 2019)
UN Photo/Loey Felipe
Mtizamo wa Baraza Kuu wakati wa ufunguzi wa kongamano la hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi mwaka 2019. (Septemba 23, 2019)

Greta Thunberg ahoji uthubutu wa viongozi kusalia na maneno huku watu wakipoteza maisha

Tabianchi na mazingira

Leo katika ufunguzi wa  mkutano wa ngazi ya juu wa viongozi wa Umoja wa Mataifa kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutrerres amesema hatakuwa mtamazaji aliye kimya kwa uhalifu ambao unaathiri hali ya sasa na  kuharibu haki kwa vizazi vijavyo kwa ajili ya mustakabali endelevu akiongeza kwamba viongozi wana haki ya kufanya kila wawezalo kukomesha janga la mabadiliko ya tabianchi kabla halijatukomesha.

Akizungumza kwenye kikao hicho Guterres, amesema mazingira yana hasira na pale yanakasirika yanajibu kwa hasira akitolea mfano ongezeko la joto, kuenea kwa ukame na ongezeko la majanga ya asili.

Licha ya hali inayoshuhudiwa kwa sasa lakini Katibu Mkuu amesema bado hajakata tamaa akisema, “nina matumaini, ni matumaini kwa sababu yenu, hili sio kongamano la mazungumzo kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Tumekuwa na mazungumzo ya kutosha, hili sio kongamano la kujadiliana, hauwezi kujadiliana na mazingira. Hili ni kongamano la hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Tangu mwanzoni, nilisema kwamba tiketi ya kuingia sio hotuba nzuri lakini hatua madhubuti. Na mko hapa na ahadi.”

Katibu Mkuu ametoa shukrani zake kwa wale wote ambao wamehudhuria mkutano ikiwemo viongozi wa serikali, sekta binafsi na vijana ambao wanatoa suluhu na kusisitiza kuhusu kutaka uwajibishwaji na hatua za haraka akisema, “kizazi changu kimeangusha sayari dunia na hilo ni  lazima libadilike akiongeza kwamba dharura ya mabadiliko ya tabianchi ni mashindano ambayo tunashindwa lakini ni mashindano tunayoweza kushinda.”

Amoengeza kwamba, “kuna gharama ya kila kitu. Lakini gharama kubwa zaidi ni kulipia ruzuku mafuta ya kisukuku, kujenga viwanda zaidi vya mkaa, na kukana kile ambacho ni wazi kama mchana, kwamba kwamba tuko katika shimo la mabadiliko ya tabianchi na ili kutoka ni lazima tuache kuchimba.”

Aidha Katibu Mkuu huyo amesema kwamba dunia inakabiliwa na kiwango cha joto kitakachoongezeka kwa nyuzi joto 3 katika kipimo cha selsiyasi ifikapo  mwishoni mwa karne hii, akisema, ‘sitakuwepo lakini, wajukuu zangu watakuwepo na vitukuu pia. Ninakataa kuwa mdau katika uharibifu wa makazi yao. Sitakuwa mtazamaji aliyekimya wa uhalifu unaoshuhudiwa katik zama za sasa na kuharibifu haki ya mustakabali endelevu. Ni wajibu wangu, wajibu wetu kufanya kila tuwezalo kukomesha janga la mabadiliko ya tabianchi kabla halijatukomesha.”

Kwa upande wake mwanaharakati kijana wa mazingira kutoka Sweden Greta Thunberg amesema uwepo wake kwenye kongamano hilo sio haki akiongeza kwamba anahitaji kuwa shuleni upande mwingine wa baharí na kwamba sayansi imekuwa wazi kwa takriban miaka 30, lakini suluhu hazipo popote.

"Tumechoka na ulaghai wenu!"

Greta akisimulia kwa hisia amesema, “mmeiba ndoto zangu na utoto wangu kwa maneno matupu na mimi ni miongoni mwa walio na bahati, watu wanakabiliwa na madhila. Watu wanakufa. Mfumo wa ikolojia inakufa. Tuko katika mwanzo wa kutokomea, na kile ambacho mnaweza kuzungumzia ni maswala ya fedha na hadithi kuhusu ukuaji wa milele wa uchumi. Mnathubutu vipi?