23 Septemba 2019

Maendeleo ya kiuchumi

Benki, kwa pamoja, zenye mali ya thamani ya dola trilioni 47, au theluthi ya sekta nzima kimataifa, jumapili zimetoa ahadi ya kuunga mkono kanuni mpya za benki zinazoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ili kukuza hatua dhidi ya tabianchi na mabadiliko kutoka mifano ya ukuaji wa uchumi "wa udhurungi hadi kijani".

Katika kanuni hizo, zilizozinduliwa siku moja kabla ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Hatua za Tabianchi mjini New York, Marekani, benki zinajikita katika kuhusisha biashara zao na malengo ya Mkataba wa Paris unaohusu mabadiliko ya tabianchi na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), na kuongeza kiwango chao cha mchango wa kufanikiwa kwa yote mawili.

"Misingi ya Umoja wa Mataifa kwa uwajibikaji katika sekta ya Benki ni mwongozo kwa tasnia ya benki ya kimataifa kujihusisha, kuendesha na kufaidika kutoka kwa uchumi wa maendeleo endelevu. Pia, yanaunda uwajibikaji unaoweza kuleta jukumu, na lengo linaloweza kusababisha hatua,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema.

UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu was Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) katika picha na kikundi na Maafisa Watendaji wakuu wa Benki wakuu wa kanuni za uwajibikaji katika Benki

Kwa kujiandikisha kwa kanuni, benki zinasema kati ya malengo mengine, zitalenga "kuongeza athari zetu nzuri, kupunguza athari mbaya, na kudhibiti hatari kwa watu na mazingira zinazosababishwa na bidhaa na huduma zetu."

“Jinsi ambavyo nyinyi viongozi wa biashara mtakavyoitikia kanuni hizi kunaweza kufafanua malengo yetu ya ulimwengu. Ni ushirikiano wa umma na wa kibinafsi tu ndio unaweza kuleta maendeleo endelevu. Tutawategemea kuongeza fedha kwa biashara zinazochochea ukuaji wa kijani. Wekeni uwaminifu katika uchumi wa kijani, sio uchumi wa kijivu, kwa maana uchumi wa kijivu hautakuwa na mustakabali,” Bwana Guterres anasema.

Akiongezea, Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), anawaeleza watu wa Benki kuwa , “wakati mfumo wa kifedha utahama kutoka kwa uwekezaji wa kahawia ulio na tamaa ya rasilimali na kwenda kwa zile za asili kama suluhisho, ndipo kila mtu atakaponufaika”.

Kanuni hizo zilitungwa na kikundi cha Benki 30 waanzilishi, kupitia ushirikiano wa ulimwengu wa ubunifu kati ya benki na Mpango wa Fedha wa UNEP, (UNEP FI).

Japo hatua  dhidi ya mabadiliko ya tabianchi inazidi kupata msukumo, bado haijafikia lengo la nyuzi joto 1.5 za  Mkataba wa Paris. Wakati huo huo, bioanuwai inaendelea kupungua kwa viwango vya kutisha na uchafuzi wa mazingira unadai mamilioni ya maisha kila mwaka.

Kinyume na msingi huu, UNEP inasema kwamba matarajio zaidi, yanayoungwa mkono na mabadiliko ya hatua ya uwekezaji kutoka kwa sekta binafsi, inahitajika kushughulikia changamoto hizi na kuhakikisha kuwa kila mtu anaishi kwa njia ambayo itahakikisha mgawanyiko sawa wa rasilimali katika mipaka ya sayari.

Sekta za kibenki na za kibinafsi zinaweza kufaidika na uwekezaji ambao wataweka katika kusaidia mabadiliko haya. Inakadiriwa kuwa kushughulikia Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kunaweza kuleta dola trilioni 12 katika akiba ya biashara na mapato kila mwaka na kuleta ajira zaidi ya milioni 380 ifikapo 2030.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud