Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio la kisiasa lapitishwa kuchochea afya kwa wote ifikapo 2030

Huduma za afya ya msingi ni pamoja na chanjo kama inavyoonekana pichani mtoto akipatiwa chanjo kwenye kituo cha afya cha kijiji cha Kombaka nchini Mali.
UNICEF/Seyba Keïta
Huduma za afya ya msingi ni pamoja na chanjo kama inavyoonekana pichani mtoto akipatiwa chanjo kwenye kituo cha afya cha kijiji cha Kombaka nchini Mali.

Azimio la kisiasa lapitishwa kuchochea afya kwa wote ifikapo 2030

Afya

Viongozi wa dunia leo wamepitisha azimio la kisiasa lenye lengo la kuhakikisha afya kwa wote ifikapo mwaka 2030. 

Tijjani Muhammad-Bande, Rais wa Baraza Kuu mkutano wa 74 akizungumza wakati wa kikao cha ngazi ya juu kuhusu Huduma za afya kwa wote UHC, tarehe 23 Septemba 2019
UN Photo/Kim Haughton
Tijjani Muhammad-Bande, Rais wa Baraza Kuu mkutano wa 74 akizungumza wakati wa kikao cha ngazi ya juu kuhusu Huduma za afya kwa wote UHC, tarehe 23 Septemba 2019

Makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Profesa Tijjani Muhammad-Bande akihoji viongozi wanaoshiriki mkutano wa ngazi ya juu kuhusu afya kwa wote iwapo wanaridhia kupitishwa kwa azimio la kisiasa kuhusu afya kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Wajumbe wakaridhia na kisha akajulisha kuwa ataliwasilisha Baraza Kuu ili lipitishwe rasmi na ndipo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akahutubia akisema kuwa ingawa afya ni haki ya kila mtu bado nusu ya wakazi wa dunia wanakosa haki hiyo ya msingi.

Hata pale inapopatikana bado inashindwa kupunguza machungu ya binadamu ikiwemo afya ya akili akisema mifumo dhaifu ya afya inaleta madhara hata nje ya mipaka akitolea mfano Ebola.

Kwa mantiki hiyo amesema“azimio hili la kisiasa ni makubaliano ya kina kuwahi kufikiwa kuhusu afya duniani- dira kwa ajili ya afya kwa wote ifikapo mwaka 2030. Haya ni mafanikio makubwa ambayo yatachochea maendeleo katika muongo ujao katika magonjwa ya kuambukiza kama vile Ukimwi, Kifua Kikuu na malaria huku ikishughulikia pia magonjwa yasiyo ya kuambukiza na usugu wa viuavijasumu kupitia mifumo thabiti ya afya ya msingi.”

Katibu Mkuu ameongeza kuwa azimio hilo pia linataka hakikisho la upatikanaji wa huduma za afya uzazi na haki za uzazi akisema kuwa, “ni muhimu kulinda ustawi na utu wa wanawake na wasichana.”

UN social Media/Priscilla Lecomte
Huzuni!

WHO YASEMA AFYA SI KWA WACHACHE AU WENGI BALI WOTE

Akizungumza naye katika kikao hicho kilichohudhuriwa na marais, mawaziri na wabunge kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema, “leo tunazitaka nchi zote ziongeze uwekezaji wake katika huduma bora za msingi za afya kwa angalau asilimia moja (1) ya pato la ndani, GDP, iwe kwa kuongeza au kuhamishia fedha kwenye huduma za afya au mambo yote mawili.”

Amesema kuwa WHO inakadiria kuwa uwekezaji wa kiwango hicho unaweza kuokoa maisha ya watu milioni 60 kila mwaka na kuongeza umri wa kuishi duniani kwa miaka 3 na miezi 7 ifikapo mwaka 2030.

Dkt. Tedros amesisitiza kuwa azimio hilo ambalo limeridhiwa na nchi wanachama ni “tamko la dunia tuitakayo.”

Amefafanua kuwa, ni dunia ambamo kwayo afya si gharama bali ni uwekezaji, dunia ambamo afya inachagiza maendeleo endelevu, dunia ambayo kila mtu atafurahia afya apaswayo kuwa nayo.

“Dira yetu si afya kwa wachache, au afya kwa wengi, bali afya kwa wote,” amesisitiza Dkt. Tedros.

Azimio hilo limepitishwa siku moja baada ya shirika la afya ulimwenguni, WHO na wadau kutoa tamkola kutaka huduma za afya ziongezwe maradufu kati ya sasa na mwaka 2030 la sivyo watu bilioni 5 watakuwa hawawezi kupata huduma za afya.

Uchunguzi wa virusi vya HIV
World Bank/Arne Hoel
Uchunguzi wa virusi vya HIV

VIPENGELE MUHIMU VINNE KATIKA AZIMIO

Kwa kupitisha azimio hilo, nchi wanachama zimeahidi kuchagize huduma ya afya kwa wote kwa kuwekeza katika maenoe manne makuu ya huduma ya afya ya msingi.

Maeneo hayo ni pamoja na kuhakikisha hakuna mtu anakumbwa na shida ya fedha kwa kutakiwa kulipia huduma ya afya kwa kutumia fedha zake na kutekeleza mikakati ya hali ya juu ya kiafha ili kukabiliana na magonjwa na kulinda afya ya wanawake na watoto.

Halikadhalika, nchi zitaimarisha nguvukazi katika sekta ya afya na miundombinu sambamba na kuimarisha usimamizi.

Hata hivyo zitatakiwa kuripotiwa maendeleo ya utekelezaji wa azimio hilo la kisiasa kwenye kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2023.

Kesho tarehe 24 mwezi huu wa Septemba, WHO na mashirika 11 ya kimataifa kwa pamoja wanaelekeza theluthi moja ya misaada ya kimaendeleo kwenye afya, watazindua mpango mkakati wa kimataifa wa utekelezaji kwa ajili ya afya na ustawi wa wote.

Mpango huo utahakikisha kuwa wadau hao 12 wanatoa msaada zaidi wa kina kwa mataifa ili yaweze kusambaza huduma ya afya kwa wote na kufanikisha malengo ya SDGs yanayohusiana na afya.