Skip to main content

Vijana bilioni 1.8 muhimu katika mustakabali wa sayari dunia

Greta Thunberg (kati kati), mwanaharakti wa maswala ya mabadiliko ya tabianchi kutoka Sweden akiungana na vijana wanaharakati katika maandamano ya kila Ijumaa kwa ajili ya kuchagiza hatua kwa mustakabali kwenye Makao Makuu ya UN Agosti 30.
UN Photo/Manuel Elías
Greta Thunberg (kati kati), mwanaharakti wa maswala ya mabadiliko ya tabianchi kutoka Sweden akiungana na vijana wanaharakati katika maandamano ya kila Ijumaa kwa ajili ya kuchagiza hatua kwa mustakabali kwenye Makao Makuu ya UN Agosti 30.

Vijana bilioni 1.8 muhimu katika mustakabali wa sayari dunia

Tabianchi na mazingira

Ni muhimu kwamba vijana bilioni 1.8 wawe na sauti kuhusu vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na hatimaye mustakabali wa sayari dunia, amesema Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya vijana Jayathma Wickramanayake.

Wanaharkati vijana, wavumbuzi, wawekezaji na waleta mabadiliko wanatarajiwa kukusanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York katika kongamano la vijana kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Septemba 21 na kushinikiza viongozi wa dunia kuchukua hatua kuzuia mabadiliko ya tabianchi.

Bi.Wickramanayake atakuwepo ambapo UN News imemuuliza ni kwa nini vijana ni muhimu kushiriki majadiliano kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa nini ni muhimu kuleta vijana pamoja kujadili mabadiliko ya tabianchi?

Kuna vijana bilioni 1.8 duniani leo, hiyo ni idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa, kwa hiyo ni muhimu wawe na sauti kuhusu mustakabali wa sayari dunia na mustakbali wao. Migomo ya kutohudhuria shule kwa ajili ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ilianzishwa na mwanaharakati kutoka Sweden, Greta Thunberg katika mji mkuu wa Sweden Stockholm na migomo hiyo na mingine kote ulimwenguni ambayo imefuatwa na vijana kote ulimwenguni, na imeonyesha kwamba wanataka hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na wanataka nafasi ya kufanya maamuzi katika mchakato wa maamuzi. Wakati wa kuchukua hatua ni sasa.

Vijana wa Afrika wako mstari wa mbele katika ujasiriamali kama inavyoonekana pichanihuko Gambia walipotembelewa na mjumbe maalum wa UN kuhusu vijana, Jayathma Wickramanayake (kulia)
Alhagie Manka/ UNFPA Gambia
Vijana wa Afrika wako mstari wa mbele katika ujasiriamali kama inavyoonekana pichanihuko Gambia walipotembelewa na mjumbe maalum wa UN kuhusu vijana, Jayathma Wickramanayake (kulia)

Kongamano la vijana linalofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa litawaleta pamoja viongozi muhimu kwa harakati ya vijana kuhusu kongamano la hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kutoa fursa kwao kuhsiriki na watu wengi zaidi. Takriban vijana 1,000 kutoka kote ulimwenguni watahudhuria tukio hilo na wengine wengi watafuatilia kwenye mtandao.

Je hilo ni dhihirisho kwamba watu walio kwenye mamlaka, au watu wazima, hawafanyi kinahohitajika?

Ni dhahiri kwamba kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kunahitaji ushirikishwaji wa kila mtu, vijana na wazee, walio nazo na walala hoi, kutoka mataifa yaliyoendelea na yale yanayoendelea. Vijana wanahitaji na wanafaa kuwa na nafasi kwa kile ambacho kinahitaji kuwa ni mchakato jumuishi na migomo ya kutohudhuria shule kwa ajili ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi zilitokana na ari ya kuwafanya viongozi wa dunia kufahamu na kuchukua hatua juu ya wasiwasi wao. Kama ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu inavyoainisha kwamba vijana ndio vinara wa maendeleo endelevu, ni wenye mawazo, ni watendaji na wabunifu ambao wanaweza kufanikisha maendeleo endelevu. Wana maslahi katika mustakabali kwani hii ndio sayari dunia watakayoirithi; ni wao ambao watakumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ni nini unafikiri kongamano la vijana linaweza kufikia?

Kongamano ni jukwaa la vijana viongozi na mashirika yanayoongozwa na vijana kuonyesha hatua ambazo wanachukua kwa ajili ya ya kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kuweka viwango vya joto katika selsiasi 1.5 juu ya viwango vya kabla ya viwanda. Mwezi Mei nilizindua changamoto yenye jina “msimu wa joto wa suluhu” kwa ajili ya vijana kubuni teknolojia za suluhu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Hii inajumuisha kutengeneza jukwaa kwa ajili ya kuwezesha taarifa za soko na hali ya hewa mashinani, kubuni vifaa vya teknolojia kwa ajili ya kuimarisha “uchumi mzunguko”, mfumo wa kiuchumi unaolenga kutokomeza taka na kutumia tena rasilimali. Mawazo mazuri yataangaziwa kwenye Kongamano la Katibu Mkuu kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Septemba 23.

Kongamano la vijana litajumuisha pia vizazi mbali mbali na kisha kuendelezwa kwenye kongamano la hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na ambalo itawezesha vijana wanaharakati kutoka mataifa ya kusini na kasakazini kuhoji viongozi wa kisiasa kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Kuwapa fursa  vijana wachanganuzi kujadili na viongozi wa kisiasa, ikiwemo kwa kuuliza maswali mazito na ya kuzua mjadala, vile vile kutoa suluhu thabiti katika jukwaa la Umoja wa Mataifa itakuwa muhimu kwani sauti za vijana zitasikilizwa. Zaidi ya hapo, na la muhimu zaidi, kwamba wanapatiwa jawabu na wanachangia katika maamuzi katika ngazi ya juu. Kongamano la vijana ni mkakati wa Umoja wa Mataifa wa hatua ya vijana kuelekea 2030 ambapo, kipaumbele cha kwanza ni ujumuishaji, ushiriki na uchagizaji kwa ajili ya kupaza sauti za vijana na kuimarisha dunia yeney amani, haki na endelevu.

Ni hatua zipi ambazo zitatokana na mazungumzo baina ya vijana na viongozi wa dunia?

Kongamano la vijana kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi zitatoa kipaumbele kwa ushirikiano na viongozi kutoka serikali za mataifa, sekta binafsi na mashirika ya kiraia. Inatarajiwa kwamba idadi kubwa ya nchi kote ulimwenguni zitadhamiria kupata mawazo ya vijana wakati wa kubuni na kutengeneza sera za hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, mipango na sheria.

Inatarajiwa pia kwamba kwa kuwezesha mijadala hiyo, viongozi wa mashirika watadhamiria kufanya kazi na kuwapa mafunzo, pamoja na kujifunza kutoka kwa vijana wawekezaji na au makampuni yanayoongozwa na vijana, wengi wa wale ambao wako mstari wa mbele katika kubuni suluhu kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Moja ya sauti muhimu kwenye kongamano la vijana, bila shaka ni Greta Thunberg. Umuhimu wake ni upi?

Vijana wanafikiria, kuhisi na kufanya vitu tofauti ukilinganisha na watu wazima na hilo ni la thamani wakati tukikabiliwa na kile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekitaja kama janga la uhai la mabadiliko ya tabainchi.

Greta Thunberg, mchagizaji wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs mwenye umri wa miaka 16 kutoka Sweden ambaye amewasili New York, Marekani Jumatano Agosti 28
UN Photo/Mark Garten)
Greta Thunberg, mchagizaji wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs mwenye umri wa miaka 16 kutoka Sweden ambaye amewasili New York, Marekani Jumatano Agosti 28

Greta Thunberg ni mfano anayetia matumaini kwa vijana kote ulimwenguni na ni ishara muhimu kwa ari yao kuchukua hatua kuzuia mabadiliko ya tabianchi. Sio jambo rahisi kusikilizwa na viongozi wa dunia kama alivyofanya, kwa hiyo kwa mantiki hiyo anabuni harakati muhimu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ikiongozwa na vijana na isiyoweza kupuuzwa. Ninafurahishwa sana na wanaharakati vijana kutoka mataifa ya kusini, ambao huenda hawaangaziwi na vyombo vya habari; kwa mfano Venessa kutoka Uganda na Timothy kutoka Fiji na maelfu ya wengine wengi ambao ni wanaharakati wanaochagiza kwa ajili ya mustakabali wa pamoja na wanaunga mkono Greta kote ulimwenguni.