WHO, UNICEF na wadau wasaidia kupambana na mlipuko wa polio Ufilipino

Afisa wa afya akitoa chanjo ya matone dhidi ya polio kwa mtoto.
UNICEF/UN018102/Al-Khatib
Afisa wa afya akitoa chanjo ya matone dhidi ya polio kwa mtoto.

WHO, UNICEF na wadau wasaidia kupambana na mlipuko wa polio Ufilipino

Afya

Shirika la afya duniani WHO, shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na wadau wengine wa afya wanashirikiana kuisaidia wizara ya afya ya Ufilipino kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa polio.

Tangazo hilo la mlipuko wa polio Ufilipino limetolewa leo na idara ya afya ya nchi hiyo DOH baada ya kisa cha polio kuthibitishwa 16 Septemba 2019 kwa mtoto wa  kike wa miaka mitatu kutoka eneo la Lanao del Sur. zaidi ya hayo sampuli za maji taka mjini Manila na mfumo wa maji mjini Davao zimethibitishwa kuwa na virusi hivyo vya polio.

Mwakilishi wa WHO nchini Ufilipino Dkt. Rabindra Abeyasinghe amesema “Tunatiwa hofu kubwa kwamba virusi vya polio sasa vinasambaa Manila, Davao na Lanao del Sur. WHO na UNICEF wanashirikiana kwa karibu na idara ya afya ili kuimarisha uchunguzi na kuchukua hatua muafaka kukabiliana na mlipuko huo. Tunawataka wazazi wote na walezi wa Watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kuwapeleka ili wapewe chanjo  waweze kulindwa dhidi ya maradhi hayo katika Maisha yao.”

Mkunga awapa chanjo dhidi ya polio Mama na mtoto wake mchanga.
Photo: UNICEF/Prashanth Vishwanathan
Mkunga awapa chanjo dhidi ya polio Mama na mtoto wake mchanga.

Naye mwakilishi wa UNICEF nchini Ufilipino Oyun Dendevnorov amesema “Ni jambo la kusikitisha kwamba virusi vya polio vimerejea tena baada ya karibu miongo miwili . Mlipuko huo unahitaji hatua za haraka ili kuwalinda Watoto Zaidi wasiambukizwe, na inatukumbusha umuhimu wa kuongeza huduma ya chanjo hadi kufikia asilimia 95 kwa Watoto kuweza kukomesha maambukizi ya virusi vya polio ambavyo mara nyingi huathiri Watoto wa umri wa chini ya miaka 5. Kwani kukiwa hata na mtoto mmoja aliyeambukizwa Watoto nchi nzima n ahata Zaidi wako katika hatari na kupata ugonjwa wa polio. UNICEF inafanya kazi kwa karibu na idara ya afya ya Ufilipino na WHO kuongeza hatua Zaidi kwa ajili ya afya na usalama wa watotonchini Ufilipino hususan katika mikoa iliyoathirika.”

Mapambano dhidi ya mlipuko wa polio

Kabla ya kutangaza mlipuko wa polio, idara ya afya ya Ufilipino na wadau wengine walizindua kampeni ya chanjo mjini Manila. Na zaidi ya hapo raundi nyingi za chanjo zinaendeshwa kwa umma kuanzia mwezi Oktoba 2019.

Mradi wa kimataifa wa kutokomeza polio GPEI unaisaidia serikali ya Ufilipino katika kupambana na mlipuko huo kwa kuwapa usauri wa kiufundi, ufuatiliaji kwenye mlipuko na mawasiliano kuhusu hatari. GPEI ni ushirika wa umma na sekta binafsi unaoendeshwa na serikali za kitaifa ukiwa na wadau wengine watano ambao ni WHO, Rotary International, Kituo cha Marekani cha kudhibiti na kuzuia magonjwa (CDC), UNICEF na wakfu wa Bill na Melinda Gates. Lengo lake ni kutokomeza polio kote duniani.