Ufadhili kwa ajili ya maendeleo ni mtihani mkubwa- Amina J. Mohammed

18 Septemba 2019

Hakuna lengo litakaloweza kutimizwa bila kuwa na fedha, lakini kuchangisha fedha za kutosha za ufadhili ni mtihani mkubwa.

Amesema naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed wakati wa mkutano na waandishi wa Habari kuhusu ripoti ya mwaka 2019 ya hali halisi ya ufadhili kwa ajili ya maendeleo na nini cha kufanya, alipozungumza nao mjini New York Marekani. Bi. Amina ameongeza kuwa  hali hiyo huongeza hatari za madeni na vikwazo vya biashara, na hii maana yake ni kwamba uwekezaji ambao ni muhimu kwa kutimiza ajenda ya 2030 hautoshelezi.

Nchini Italia, mvulana, amesimama nje katika mtaa duni katika mji wa Turin, eneo la Piedmont.
UNICEF/UNI173328/Pirozzi
Nchini Italia, mvulana, amesimama nje katika mtaa duni katika mji wa Turin, eneo la Piedmont.

 

Naibu Katibu Mkuu amesema ripoti ya ufadhili kwa ajili ya maendeleo endelevu iliyotolewa Aprili mwaka huu ina takwimu za kutia hofu kwani “inaonyesha kwamba ingawa uchumi umekuwa kwa asilimia 3, mishahara ya watu imeshuka kwa asilimia 1.8 ambacho ni kiwango cha chini kwa zaidi ya mwaka mmoja, pengo la usawa linazidi kupanuka, nchi 30 zinazoendelea ziko katika hatari au zinaelekea katika hatari kubwa ya mzigo wa madeni, uwekezaji katika nchi zinazoendelea uko chini kuliko ilivyokuwa mwaka 2012,  na ingawa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje kwenda kwenye nchi zinazoendelea umeongezeka lakini uwiano wake si sawa katika nchi zote na zaidi ya hapo tunashuhudia mabadiliko ya tabianchi yakizitishia nchi zote katika utimizaji wa SDGs.”

Changamoto iliyopo

Mtihani uliopo sasa amesema Bi. Amina ni kushinika nchi zote kukumbatia ahadi ya kuongeza ufadhili wa maendeleo kwa lengo la kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya ajenda ya mwaka 2030 na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.

 

Mambo matano muhimu ya kuzingatia

Naibu Katibu mkuu amesema tathimini ya mwaka huu imekuja na ujumbe maalum wa mambo matano ya muhimu y kuyatilia maanani.

“Mosi mfumo wa ushirikiano wa kimataifa uko katika shinikizo kubwa na unabadili haraka mazingira ya kimataifa na hii inazilazimisha nchi kufanya marekebisho mfumo wa sasa wa ushirikiano wa kimataifa na pia kufungua mlango zaidi wa taasisi za ushirikiano wa kimataifa kukidhi haja inayohitajika. Pili katika kukabiliana na hali hiyo jumuiya ya ushirikiano wa kimataifa ni lazima ifanye ahadi tena ya kuchukua hatua hatua ya kuunda tena mfumo wa ufadhili kwa mfano kutafuta hatua ya kufuta mzigo wa madeni, kanuni za kodi, na hususan mfumo wa ushirikiano wa biashara, hii ni changamoto kubwa lakini haizidi mbinu na uwezo tulionao. Sasa hivi majadiliano yanaendelea katika maeneo yote haya, lakini swali linabaki ni mfumo gani tutakaokuwa nao? Badala ya kuondokana na ushirikiano wa kimataifa ni  lazima tuimarishe hatua zetu za pamoja na kusaidia maendeleo endelevu. Tatu mtazamo wa kimataifa lazima uende sanjari na hatua za kitaifa , tunazichagiza nchi kuwa na mfumo madhubuti ambao utasaidia kuweka vipaumbele katika mfumo wa ufadhili kwa ajili ya maendeleo. Mfumo wa ufadhili wa kitaifa ulizinduliwa katika ajenda ya Addis Ababa na sasa ni wakati wa kuanza kutumia ajenda hizo kwa ajili ya ufadhili endelevu mashinani. Nne kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi inahitali mtazamo wa muda mrefu . Sekta binafsi na sekta za umma zinatakiwa kwenda sanjari na mikakati hiyo ya muda mrefu , mtazamo wa muda mrefu wa masuala ya mikopo , kuweka kodi ya juu kwa bidhaa zinazozalisha hewa ukaa. Tano na mwishi ni lazima tuboreshe umuhimu wa ubunifu katika ufadhili wa maendeleo.Watu nusu bilioni wamepata fursa ya ufadhili wa fecha katika miaka ya karibuni na kiasi kikubwa ni kutokana na teknolojia ya mafsuala ya fedha , hii pia imerahisisha mfumo wa malipo kwa kadri unavyotumia ,a malipo kabla ya matumizi hususani katika sekta za nishati hali ambayo imesaidia kusongesha utekelezaji wa SDGs. Lakini pia imeleta hatari ambazo zinapaswa kushughulikiwa kwa kina . Ripoti imetoa wito wa kutathimini hatari hizo na kuzitafutia uvumbuzi ikiwemo ukuaji wa teknolojia ya masuala ya fecha.”

Mjadala wa ngazi ya juu kuhusu ufadhili kwa ajili ya maendeleo utakaofanyika Septemba 26 utawaleta pamoja viongozi wa nchi, wafanyabiashara na sekta za fedha, kwa dhamira ya kusaka rasilimali na ushirika unaohitajika na kusongesha mbele mchakato wa maendeleo. Inakadiriwa kwamba uwekezaji wa takriban dola trilioni 5 hadi 7 unahitajika kila mwaka katika sekta zote ili kufikia malengo ya SDGs, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatoa wito wa kuweka mazingira ambayo yatawezesha uwekezaji wa muda mrefu katika maendeleo endelevu, kuchagiza afya na mustakabali wa watu wote na sayari dunia.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter