Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Acheni kutumia vilipuzi kwenye maeneo ya raia: UN, ICRC

Watoto wanaokimbia machafuko Idlib watafuta hifadhi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani karibu na kijiji cha Atmeh.
UNICEF/Watad
Watoto wanaokimbia machafuko Idlib watafuta hifadhi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani karibu na kijiji cha Atmeh.

Acheni kutumia vilipuzi kwenye maeneo ya raia: UN, ICRC

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, ICRC Peter Maurer, wametoa taarifa ya pamoja kuhusu ya kusihi kuachwa kwa matumizi ya vilipuzi kwenye miji wakisema kuwa huleta machungu kwa raia.

Taarifa hiyo ya pamoja imetolewa leo jijini New York, Marekani na Geneva, Uswisi ikitolea mfano miji ya Idlib nchini Syria na Tripoli nchini Libya ambako sasa hivi makombora na mabomu yanarushwa kila kona na kusababisha uharibifu wa miundombinu na madhara kwa raia.

Wametaja pia miji mingine ambayo hivi karibuni ilikumbwa na madhila hayo, miji hiyo ni Mosul na Fallujah nchini Iraq, Aleppo, Raqqa nchini Syria, Taiz na Sana’a huko Yemen na Donetsk nchini Ukraine.

Hata hivyo wamesema licha ya madhila hayo, ni nadra sana matukio hayo kugongwa vichwa vya habari wakisema kuwa, “matukio ya vita mijini hayapaswi kuripotiwa kwenye kurasa za nyuma za vyombo vya habari, ni kwamba hivi sasa watu milioni 50 wanakabiliwa na madhara ya mashambulizi hayo.”

Ni kwa mantiki hiyo ICRC na Umoja wa Mataifa wanataka pande husika kwenye mizozo ya kivita ziepushe kutumia vilipuzi kwenye maeneo ya makazi ya watu.

“Kadri maeneo ya miji yanavyopanuka duniani, halikadhalika mizozo. Pindi miji inavyoshambuliwa kwa mabomu na makombora, raia wanabeba mzigo zaidi. Ni kwamba idadi kubwa ya waathirika, sawa na asilimia 90 ni raia,” imesema taarifa hiyo ya Guterres na Maurer.

Wamesema kuwa picha za kutisha kutoka makazi ya raia huko Afghanistan, Iraq, Syria, na Ukraine huonyesha mwenendo madhara makubwa kwa raia ambayo mtu huwezi kupuuza lakini mara nyingi husahaulika.

Wawili hao wamesema pande kwenye mzozo zinapaswa ku tambua kuwa hazipaswi kufanya mapigano hayo kwenye maeneo ya raia kama vile wanavyofanya kwenye uwanja wa vita.

“Zinapaswa kutambua kuwa kutumia vilipuzi na mabomu kwenye maeneo ya miji na kambi za wakimbizi huweka raia katika hali tete kwa kuwa ni vigumu kufanya mashambulizi ya kulenga upande mmoja katika maeneo hayo,” imesema taarifa hiyo.

Wametoa mfano wa madhara huyo Yemen ambako mwezi uliopita pekee kwenye mji wa Aden, watu wapatao 200,000 walikosa huduma ya maji safi na salama baada ya mapigano makali kuharibu miundombinu ya maji.

Kwa mantiki hiyo wametaka serikali kuridhia sera na kanuni za kulinda raia kwenye mizozo ikiwemo zile za kuepusha matumizi ya vilipuzi.