Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marufuku ya plastiki za kutumia na kutupa UN ni moja ya mafanikio yangu- Maria Espinosa

Maria Fernanda Espinosa, Rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika mahojiano na Eleuterio Guevane wa Idhaa ya Kireno ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.  (Septemba 2019)
UN News/Daniela Gross
Maria Fernanda Espinosa, Rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika mahojiano na Eleuterio Guevane wa Idhaa ya Kireno ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. (Septemba 2019)

Marufuku ya plastiki za kutumia na kutupa UN ni moja ya mafanikio yangu- Maria Espinosa

Masuala ya UM

Rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaotamatishwa hii leo, María Fernanda Espinosa ametaja marufuku ya plastiki zinazotumiwa mara moja na kutupwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kuwa moja ya mafanikio makubwa ya kipindi chake.

Bi. Espinosa amesema hayo wakati akijibu swali la Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu mafanikio ya kipindi chake kinachofikia ukingoni hii leo.

Amesema kampeni hiyo kwenye makao makuu ya UN sambamba na kule visiwa vya Karibea ni jambo mujarabu na kwamba, “kampeni ya kuleta pamoja zaidi ya watu milioni 400 ambao sasa wanatambua kuwa tunateketeza bahari zetu kwa kutumia plastiki mara moja na kuzitupa, kampeni ambayo pia iliwezesha serikali za Karibea kuamua kuungana na kupiga marufuku matumizi ya plastiki hizo.”

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake na haki za wanawake akisema kuwa, “kila kitu nilichofanya, kila ziara niliyokwenda, kila kikao cha ngazi ya juu, mjadala au mashauriano yalikuwa na hoja hiyo ya uwezeshaji wanawake na usawa kama kitovu na kama ujuavyo niliunda kundi la washauri wa masuala ya jinsia kutoka kila ukanda.”

María Fernanda Espinosa, Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la UN katika mkutano wake wa mwisho na wanahabari New York, Marekani 16 Septemba 2019
UN Photo/Cia Pak
María Fernanda Espinosa, Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la UN katika mkutano wake wa mwisho na wanahabari New York, Marekani 16 Septemba 2019

Nilitaka nithibitishe kuwa uteuzi wangu ni sahihi

Alipoulizwa fikra zake kuhusu yeye kuwa miongoni mwa wanawake wachache waliowahi kushika wadhifa wa urais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na wa kwanza kutoka Amerika ya  Kusini, Bi. Espinosa amesema ilikuwa ni  heshima kubwa na changamoto kwa sababu alitambua lazima atimize majukumu yake na adhihirishie nchi wanachama kuwa yeye alikuwa mtu sahihi na pia alikuwa mwanamke.

Akifafanua zaidi amesema, “kwa hiyo nadhani, kimsingi ujumbe ni kwamba tunapaswa kuwa na wanawake zaidi kwenye uongozi. Hatuwezi kuendelea kuwa na asilimia 75 ya wabunge wanaume, wanawake ambao ni wakuu wa nchi na serikali ni 21 tu kati ya viongozi 193, kwenye maafisa watendaji wa kampuni 500 kubwa wanawake ni chini ya asilimia 5 tu. Kwa hiyo namba haziko sawa, ikimaanisha kuwa ubora wa utawala si sawa. Idadi sawa ya jinsia kwenye uongozi si tu haki bali pia ni jambo maarifa ya kawaida.”

Bi. Espinosa amekumbusha kuwa wanawake wanapaswa kuwa kitovu cha sera za umma, kuanzia ngazi za mashinani hadi za kimataifa, “hata hivyo hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa kwa sababu bado wanawake na wasichana wanakandamizwa.”

Je UN bado ina nafasi katika zama za sasa?

Idhaa ya Umoja wa Mataifa ikataka kufahamu mtazamo wake kuhusu dhima ya Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya amani na usalama hasa wakati huu bado kuna masuala lukuki hayajapatiwa ufumbuzi ikiwemo mzozo kati ya Israeli na Palestina.

Bi. Espinosa katika kujibu swali hilo amesema ni dhahiri  ya kwamba katika safari zake amekuwa akizungumza na makundi ya vijana na wanawake ambao, “kila wakati wanataka kuona Umoja wa Mataifa unatekeleza majukumu yake kwa usawa. Lakini Umoja wa Mataifa ni sisi sote tukifanya kazi pamoja n ani kweli kuwa tuna mizozo ambayo inazidi kwa wigo na ugumu na mingine inadumaa.”

Amesema ni lazima kukikri kuwa mzozo wa Israel na Palestina umekwama na kinachotakiwa ni kuchukua hatua akisema kuwa, “kwa sababu tuna maazimio ya Baraza la Usalama, maazimio lukuki ya Baraza Kuu. Huu ni wakati wa kuyatekeleza. Nadhani Umoja wa Mataifa ni pahala pekee ambako hata mizozo iliyodumu inaweza kutatuliwa kupitia mashauriano ya kisiasa yenye suluhu za amani.”

Mfuko wa plastiki.
UNnewskiswahili/Patrick Newman
Mfuko wa plastiki.

Katibu Mkuu Guterres ampongeza Bi. Espinosa kwa mchango dhidi ya plastiki

Alasiri ya tarehe 16 Septemba 2019, kumefanyika tukio rasmi la kukunja jamvi la mkutano wa 73 wa Baraza  Kuu ambapo Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye alitumia fursa hiyo kumpongeza Bi. Espinosa kwa jinsi alisimamia kidete suala la kutokomeza matumizi ya plastiki.

“Azma ya Bi. Espinosa kwa upande wa mazingira na hususan kutokomeza matumizi ya plastiki za kutumia na kutupa hili limeng’ara zaidi. Ninaamini kuwa awamu yake ya mafanikio makubwa inafungua njia kwa ushiriki zaidi wa wanawake kwenye medani za kisiasa duniani kote na kuchagiza maendeleo kuelekea usawa wa jinsia ndani ya Umoja wa Mataifa na nje,” amesema Bwana Guterres.

Amegusia pia kupitishwa kwa mikataba miwili wakati wa mkutano wa 73, mikataba ya kimataifa ule wa wakimbizi na ule wa wahamiaji akisema ni mifano ya kipekee.

Katibu Mkuu amesema “tunaendelea kuhakikisha shirika letu linakwenda na wakati, linakuwa fanisi na lenye tija ili liweze kuhudumia zaidi wakazi wa dunia yetu,” akiongeza kuwa “tunavyoelekea kuadhimisha miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, namshukuru Bi. Espinosa kwa uongozi wake na ubia na nasubiri kwa hamu kufanya kazi kwa ushirikiano na Rais-mteule wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu Balozi Tijjani Muhammad-Bande, kutoka Nigeria.

Wakati wa mkutano wa 73, Baraza Kuu lilipitisha zaidi ya maazimio 340 yakiwa na ajenda zaidi ya 178, ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu mwaka 2001.

Miongoni mwa mambo muhimu ni kuunga mkono kampeni ya kimataifa dhidi ya plastiki zinazotumiwa mara moja na kutupwa, vikao vya ngazi ya juu kuhusu masuala ya wanawake na uongozi, na suala la kusongesha ajenda ya ushirikiano wa kimataifa.

Kumalizika kwa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu kunaashiria kufungua pazia kwa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu hapo kesho Septemba 17 mwaka 2019 ambapo Rais wa mkutano huo ni Balozi  Tijjani Mohammad Bande kutoka Nigeria.

Rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la UN Maria Espinosa (kulia) akimkabidhi Rais wa mkutano 74 wa Baraza Kuu Balozi Tijjani Muhammad-Bande (kushoto) rungu la kuongozea kikao. Anayetazama kwa mbali ni Katibu Mkuu Antonio Guterres.
UN /Loey Felipe
Rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la UN Maria Espinosa (kulia) akimkabidhi Rais wa mkutano 74 wa Baraza Kuu Balozi Tijjani Muhammad-Bande (kushoto) rungu la kuongozea kikao. Anayetazama kwa mbali ni Katibu Mkuu Antonio Guterres.