Mwanamke aliyebakwa na wanaume 17 Sudan Kusini ahoji kazi ya kamisheni ya haki za binadamu

16 Septemba 2019

Mmoja wa wanawake waliobakwa mara kadhaa na magenge ya wahalifu huko Sudan Kusini amehoji ni hatua gani zitachukuliwa na kamisheni hiyo na jamii ya kimataifa ili kumnusuru yeye na wanaweke wengine waliokumbwa na madhila kama hayo huko Bentiu.

Hoja ya mwanamke huyo imewasilishwa hii leo huko Geneva, Uswisi mbele ya wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na mwenyekiti wa kamisheni ya haki za binadamu kwa ajili ya Sudan  Kusini, Yasmin Sooka.

Bi. Sooka alikuwa akiwasilisha kile yeye na wajumbe wenzake wawili walishuhudia na kusimuliwa na wanawake wa Bentiu akisema mwanamke huyo alimweleza kuwa alibakwa mwaka 2014 na kisha akabakwa na wanaume 6 na siku chache baadaye alibakwa na askari 10 karibu na kituo cha makazi ya wakimbizi wa ndani.

Amesema kutokana na kubakwa mara kadhaa na magenge, hivi sasa mwanamke  huyo mwenye umri wa miaka 60 amepata tatizo la kizazi chake kushuka hadi ukeni na hawezi kujihudumia na hivyo Bi. Sooka anataka hatua zaidi zichukuliwe kusongesha makubaliano mapya ya amani na pia usaidizi kwa manusura wa ukatili huo.

Kuhusu vurugu zinazodaiwa kufanywa na majangili, Bi. Sooka amesema cha kushangaza majangili hao hawatumii fimbo kama zamani bali wana silaha za kisasa kama AK-47 na makombora akisema..

(Sauti ya Yasmin Sooka)

“Katika matukio mengine, silaha hizi zinaripotiwa kusambazwa na mamlaka za mitaa na wanasiasa wanatumia wafugaji kama vikundi vyao vya mbali. Lengo lao la kuiba mifugo linaweza pia kuwa kushinikiza kabila fulani likimbie, waue viongozi wa kijamii na kuteka wanawake na watoto, na kuchoma nyumba na kupora na kuharibu vitu na hii hatimaye inaweza kuwa jambo baya zaidi.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter