Demokrasia ni kuhusu watu, tuheshimu hilo:Guterres

15 Septemba 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema demokrasia ni kuhusu watu na hivyo ni muhimu sana kuheshimu hilo.

Katika ujumbe wake maalumu kuhusu siku ya kimataifa ya Demokrasia ambayo kila mwaka huadhimishwa Septemba 15, Antonio Guterres amesema "moyoni, demokrasia ni kuhusu watu. Inajengwa na ujumuishi, kutenda usawa na ushiriki na ni msingi muhimu kwa ujenzi wa amani, maendeleo endelevu na haki za binadamu."

 

Ameongeza kuwa maadili na matakwa haya yasionekane tu kama ishara au maneno matupu. Lazima yadhihirike katika maisha ya watu.

Hata hivyo amesema " bado Siku ya Kimataifa ya Demokrasia inafanyika katika wakati huu ambapo uaminifu uko chini na hofu iko juu.Watu wanasikitishwa na kuongezeka kwa pengo la usawa na kuvurugwa na mabadiliko yanayojitokeza kutokana na utandawazi na teknolojia."

Amesema wanaona migogoro ikiendelea bila kutatuliwa, dharura ya mabadiliko ya tabianchi ikiendelea bila kujibiwa, ukosefu wa haki unaendelea bila kushughulikiwa, na fursa za raia zikipungua.

 

Hivyo amesisitiza kuwa "Tunapoadhimisha Siku ya Demokrasia, ninazisihi serikali zote kuheshimu haki ya kushiriki kikamilifu; na ninawapongeza nyote ambao mnajitahidi bila kuchoka kuhakikisha haya yanafanyika."

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud