Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yaonya bila hatua za haraka watoto milioni 12 hawatowahi kutia mguu shuleni

Watoto darasani Sakassou, Côte d'Ivoire.(8 Julai 2019) Chris Mburu anapigania elimu nchini mwake Kenya akiamini elimu ndiyo ufunguo wa kila kitu maishani
© UNICEF/Frank Dejo
Watoto darasani Sakassou, Côte d'Ivoire.(8 Julai 2019) Chris Mburu anapigania elimu nchini mwake Kenya akiamini elimu ndiyo ufunguo wa kila kitu maishani

UNESCO yaonya bila hatua za haraka watoto milioni 12 hawatowahi kutia mguu shuleni

Utamaduni na Elimu

Takwimu mpya zilizochapishwa leo na kitengo cha takwimu cha shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCOkuhusu Watoto wasiohudhuria shule zinaonyesha kwamba hakuna hatua yoyote iliyopigwa au kuna hatua ndogo sana ilipyopigwa kwa zaidi ya muongo mmoja.

 

Kitengo hicho cha takwimu UIS, kimesema takriban watoto milioni 258, barubaru na vijana hawakuhudhuria shule mwaka 2018 kote duniani ambao wana umri wa miaka 6-17 umri wa kwenda shuleni.

Takwimu zinaonya kwamba cha kuogopesha zaidi ni ukweli kwamba hatua madhubuti na za haraka zisipochukuliwa watoto milioni 12 wa umri wa kuhudhuria shule za msingi hawatowahi kutia mguu shuleni. Na hii itakuwa ni vigumu sana kuhakikisha ujumuishi na elimu bora kwa wote ambalo ni lengo mojawapo la maendeleo endelevu SDGs linalopaswa kutimia ifikapo 2030.

Takwimu hizo zinakadiria kwamba katika kiwango cha sasa mtoto mmoja kati ya sita hawatohudhuria ekimu ya msingi na sekondari ifikapo 2030 na kwamba ni Watoto 6 tu kati ya 10 ndio watakaomaliza elimu ya sekondari.

Pengo katika elimu

Takwimu hizo pia zimedhihirisha pengo kubwa lililopo baina ya nchi tajiri na masikini ambapo Watoto wa umri wa miaka 6 hadi 11 asilimia 19 hawahudhurii shule katika nchi za kipato cha chini ikilinganishwa na asilimia 2 tu katika nchi tajiri na pengo ni kubwa Zaidi kwa barubaru na vijana ambapo alimia 61 ya vijana wa umri wa miaka 15 na 17 hawahudhurii shule katika nchi masikini ikilinganishwa na asilimia 8 katika nchi tajiri.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay,”wasichana wameendelea kukabiliwa na vikwazo vikubwa huku makadirio yakionyesha kwamba wasichana milioni 9 wa umri wa shule za msingi hawatowahi kuanza shule au kutia mguu darasani ikilinganishwa na wavulana ambao ni milioni 3.”

Na wasichana milioni 4 kati ya hao milioni 9 wanaishi katika nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la sahara ambako hali inatia hofu kubwa.Hivyo Bi Silvia Montoya mkurugenzi wa UIS  amesema “ni lazima tuendelee kutia msukumo wa hatua zetu kwa elimu ya wasichana na wanawake kama kipaumbele.Tuna miaka 11 tu ya kuhakikisha tunatimiza ahadi ya kila mtoto kupata elimu, na badoo takwimu zinaonyesha hakuna mabadiliko ya fursa ya kupata elimu bora mwaka hadi mwaka.”

Amesema hili litawezekana kwa mchanganyiko wa hatua madhubuti na ufadhili wa kutosha. Zinahitajika ahadi za vitendo kutoka kila serikali na wafadhili kuhakikisha kazi inafanyika na ahadi inatimizwa.

Takwimu hizo zimetoka siku chache tu kabla ya Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kukutana kutathimini hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa SDGs.