UN yazindua mkakati kulinda maeneo ya dini na waumini wake

12 Septemba 2019

Baada ya jitihada ka kazi kubwa ya miezi kadhaa iliyosimamiwa na mwakilishi wa ngazi ya juu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Muungano wa ustaarabu Miguel Moratinos, leo Umoja wa Mataifa umezindua mpango wa hatua kwa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuyalinda maeneo ya kidini na waumini wake.

Akizungumza katika uzinduzi wa mkakati huo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres amesema “sote tunatambua kwamba dunia yetu hivi sasa inaghubikwa na wimbi la chuki dhidi ya Wayahudi, chuki dhidi ya Uislam, mashambulizi dhidi ya wakristo na hali ya kutovumiliana inayowalenga watu wa makundi mengine ya kidini.” 

Hivyo umewadia wakati wa kuchukua hatua kukomesha hali hiyo kwa mkakati maalum na Umoja wa Mataifa umnafanya hivyo kwa kuwashirikisha wadau wote zikiwemo serikali, viongozi wa kidini, mashirika ya kidini, asasi za kiraia, vijana wa kike na wa kiume, jamii, vyombo vya Habari vya asili na mitandao ya kijamii na pia sekta binafsi.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa “Leo hii tunazindua mkakati ambao unatekelezeka, mkakati wa Umoja wa Mataifa wa hatua ili kulinda waeneo ya kidini. Mpango huu unatoa mapendekezo ya kuzisaidia nchi wanachama katika juhudi zao za kuhakikisha kwamba maeneo ya kidini yako salama, ambayo waumini wanaweza kuendesha sala zao kwa amani na kwamba thamani ya ut una kuvumiliana inakumbatiwa duniani kote.”

UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiweka shada la m aua huko Christchurch New Zealand kuenzi waathirika wa shambulio la Machi mwaka huu.

Amesema mpango huo umetokana na azimio la kimataifala haki za binadamu na mizizi yake ni kanuni saba za muongozo ambazo ni: Mosi heshima kwa wote, pili wajibu wa kujenga daraja la maelewano na ushirikiano, tatu jinsi ya kukubali la kuheshimu tofauti miongoni mwa wanadamu, nne majadiliano kama nyenzo ya kuwasiliana vyema na kuhusiha kila mmoja, tano mshikamano ili kusaidiana hususan katika wakati wa majonzi au matatizo, sita kusimama pamoja kama kitu kimoja kuchukua hatua dhidi ya majaribio ya kutugawanya na saba kukaa pamoja kama kitu kimoja ili kuhakikisha umoja huo katika kukabiliana na mashambulizi dhidi ya maeneo ya kidini unasimamiwa na kuimarishwa kwa muda.

Na juhudi hizo zinaenda sanjari na mkakati na mpango wa hatua kuhusu hotuba za chuki uliozinduliwa mwezi June mwaka huu.

Guterres amesema “maeneo ya kidini ni ishara zenye nguvu za ufahamu wetu wa pamoja. Wakati watu wanaposhambuliwa kwa sababu ya dini au imani zao, jamii yote huathiriwa. Nyumba za ibada kote duniani ni lazima ziwe mahala salama pa kutafakari na amani na sio maeneo ya kumwaga damu na ugaidi.”

Amesisitiza kwamba watu kila mahali wanapaswa kuruhusiwa kufuata na kutimiza imani zao kwa amani.

Na katika hali za vita amesema majengo yaliyowekwa maalumu kwa ajili ya dini yanalindwa na sheria za kimataifa za kibinadamu, kwani “mashambulizi ya kimataifa dhidi ya majengo hayo ni uhalifu wa vita na tayari mahakama ya kimataifa ya uhalifu imeshamuhukumu mtu kwa kutekeleza uhalifu huo.”

Amehimiza kuwa njia bora zaidi ya kukabiliana na hatari ya vitisho vya machafuko katika mundo usiokubalika dhidi ya dini na imani za kidini ni kuungana kupaza sauti zetu kupinga ujumbe wa chuki kwa kutoa ujumbe wa amani, kukumbatia tofauti zetu kama ni faida na sio tishio, kuwekeza katika mahusiani ya kijamii na kulinda haki za binadamu.

“Kwa pamoja tunaweza kuzuia mashambulizi dhidi ya maeneo ya kidini na kufanya tuwezalo kuhakikisha usalama wa kuabudu kwa amani.”

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter