Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utamaduni na chakula ni chachu ya kutimiza SDGs:UNESCO

Hapa ni kwenye moja ya soko nchini Thailand, wadudu wakiuzwa kama kitoweo.
P.B. Durst
Hapa ni kwenye moja ya soko nchini Thailand, wadudu wakiuzwa kama kitoweo.

Utamaduni na chakula ni chachu ya kutimiza SDGs:UNESCO

Utamaduni na Elimu

Kongamano la kimataifa lililoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataoifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO limeanza leo mjini Parma Italia likimulika jinsi gani chakula na utamaduni vinavyoweza kutoa suluhu ya changamoto zinazoikabili dunia za ongezeko la idadi ya watu duniani, mabadiliko ya tabianchi na jukwaa kwa ajili ya majadiliano ya jamii jumuishi. 

Kongamano hilo “Utamaduni na chakula:mikakati bunifu kwa ajili ya maendeleo endeleo” ni la siku mbili na limewaleta pamoja washiriki na wazungumzaji zaidi ya 150 ambao watajikita katika masuala makuu matatu ambayo ni mosi kutathimini tafiti zilizopo na sera, hatua na ushiriki katika masuala ya utamaduni na chakula wakihusisha wadau muhimu. Pili watabaini fursa muhimu zizlizopo na changamoto na tatu kudodosa njia bunifu ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu yaani SDGs.

Kwa mujibu wa UNESCO utamaduni na chakula viko katika njiapanda ya mila na ubunifu na hivyo kongamano hilo litachambua uhusiano uliopo baina ya chakula, utamaduni na jamii , lakini pia mabadiliko katika uhakika wa chakula na mifumo ya chakula  na jukumu lake muhimu katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya 2030.

Shirika hilo limesisitiza kwamba “chakula daima kimekuwa kikiunda uhusiano wetu na mazingira tangu mwanzo wa jamii za wakulima hadi wakati wa maendeleo ya viwanda ya karne ya 21.”

Ukirithishwa kutoka kikazi hadi kizazi mchakato wa kukusanya chakula, kukiandaa na kukihudumia ni sehemu ya urithi wa utamaduni wetu unaoigusika na usiogusika n ani chanzo cha asili yetu ambapo kila mlo ni wa kipekee ukjidhihirisha historia, muundo wa Maisha, thamani na imani zetu.

Hata hivyo mapishi hayakusalia kama awali , yamevuka mipaka na mabara na kutumika kama njia ya majadiliano ya tamaduni tofauti.

UNESCO inasema kuchagiza vyakula tofauti, mabadiliko ya tabia ili kuhakikisha matumizi endelevu na kuepuka utupaji chakula, pamoja na mfumo wa Maisha ni vipengee muhimu vya mkakati wa kimataifa wa kufikia SDGs.

Kongamano hilo la UNESCO lililoandaliwa kwa ushirikiano na serikali ya Italia linahakikisha utamaduni na chakula ndio maneno yanayopewa kipaumbele kupitia mikutano na majadiliano mbalimbali yatakayowahusisha washiriki, wataalam wa kimataifa, wapishi, wawakilishi wa serikali, asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali au NGOs na litakunja jamvi kesho Septemba 13.