Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali katika kambi ya Al Hol Syria si ya kibinadamu-Kamisheni ya UN

Wakimbizi wa Syria wakiwa mbioni kutafuta makazi
UNICEF/UN0277723/Souleiman
Wakimbizi wa Syria wakiwa mbioni kutafuta makazi

Hali katika kambi ya Al Hol Syria si ya kibinadamu-Kamisheni ya UN

Haki za binadamu

Wakati watu wa kaskazini Magharibi mwa Syria wakikabiliwa na ongezeko la vurugu, maelfu ya wanawake na watoto wanaendelea kuwekwa katika “hali mbaya ya kibinadamu” kambini katika upande mwingine wa nchi, wameeleza hii leo mjini Geneva Uswisi wachunguzi wa Umoja wa Mataifa.

Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Syria ikieleza hali ilivyo katika kambi ya Al Hol, wamesema ni hali ya kutisha na wakaitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua.

Watoto wengi kati ya watoto 3,500 wanaoshikiliwa katika kambi wanakosa nyaraka za usajili wa kuzaliwa, kamisheni imesema katika ripoti kuhusu mgogoro unaoendelea nchini Syria

Mwenyekiti wa jopo la kamisheni Bwana Paulo Pinheiro ameeleza kuwa watoto hao wako hatarini kwasababu nchi wanachama wanaonekana kutokuwa tayari kuwapokea kwa kuhofia kuhusishwa na makundi ya kigaidi.

Pinheoro amesema, “hadi kufikia watu 70,000 wamebaki kizuizini katika hali mbaya isiyo ya kibinadamu katika kambi ya Al Hol, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto chini ya umri wa miaka 12.”

Akitoa ombi kwa niaba yao, ameongeza, “watoto kuanzia umri wa miaka 12 hadi 18 ni watoto na barubaru na tunafikiri kuwa inashangaza…mnafahamu hao watoto waliko? Hatufahamu; pengine mnaweza kuwauliza nchi wanachama mahali waliko hawa vijana na wanafikiriwa kuwa ni magaidi ikiwa wana umri wa zaidi ya miaka 12. Kamisheni inaona hii inatisha.”

Kambini Al Hol
OCHA/Hedinn Halldorsson
Kambini Al Hol

 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kamisheni, misaada ya kibinadamu kwa mahitaji ya kambi ya Al Hol haitoshi huku vifo ambavyo vingezuilika vikitokea.

Takribani watoto 390 wamefariki dunia kutokana na utapiamlo au majeraha ambayo hayakutibiwa, wachunguzi wamesema.

Ripoti imeshauri pia kuwa msaada wa kisaikolojia unahitajika sana lakini unatolewa kwa kiwango kidogo kwa wanawake na watoto wa Yazidi ambao walikimbia mauaji ya kundi la ISIL katika nchi jirani ya Iraq mnamo mwaka 2014.

Idadi kubwa pia ya wale wanaoshikiliwa katika kambi ya Al Hol ni pamoja na maelfu ya watu ambao walikimbia mashambulizi ya mabomu katika mji wa Baghouz, ngome ya ISIL huko  mashariki mwa Syria, na hivyo kuongeza mzigo kwa misaada ya kibinadamu ambayo tayari imelemewa.