Ufadhili zaidi unahitajika kukabiliana na changamoto za mara kwa mara Ethiopia- OCHA

10 Septemba 2019

Ethiopia inakabiliwa na changamoto za mara kwa mara na za sura tofauti za kibinadamu na ufadhili zaidi unahitajika kutoka kwa jamii ya kimataifa pia msaada kwa juhudi za serikali kwa ajili ya janga la watu kufurushwa makwao.

Hiyo ni kauli ya Mkuu wa misaada ya dharura kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Mark Lowcock.

Taarifa hii ni kufuatia ziara ya bwana Lowcock ya siku mbili nchini Ethiopia amabapo amesema watu zaidi ya milioni nane nchini humo wanahitaji chakula, makazi, dawa na msaada mwingine wa dharura. Ameongeza pia, “ukame na mafuriko, milipuko ya magonjwa na ukatili wa kikabila katika miaka ya hivi karibuni vimelazimisha mamilioni ya watu kukimbia makwao.”

Bwana Lowcock ambaye aliandamana na afisa wa ujenzi wa amani wa Umoja wa Mataifa , Oscar Fernandez-Taranco, na mtaalum huru wa Umoja huo kuhusu wakimbizi wa ndani Cecilia Jimenez-Damary wamekutan na famili waliorejea makwao hivi majuzi na watu katika maeneo yaliyoathirikia na vita ikiwemo watu wa Chitu Kebele katika wilaya ya Yirgachefe, Gedeo, moja ya eneo linaloathiriwa na machafuko ya kikabila ambayo yamepelekea watu kuhama na wengine kupoteza maisha tangu 2018.

Mkuu huyo wa OCHA amesema, “ninaunga mkono azma ya serikali kutafuta suluhu ya kudumu kwa ajili ya changamoto ya wakimbizi na ninaelewa namna hilo ni ligumu kusuluhisha.” Ameongezwa kwamba, “ wakati watu wengi sasa wameweza kurudi makwao, wengine wanasalia katika njia panda, wakiishi karibu na nyumba zao zilizoharibiwa wakisikitika kwamba hawatokuwa na fursa ya kuanza upya kilimo na vitega uchumi vyao walivyopoteza walipokimbia mwaka jana.”

Bwana Lowcock ameongeza kuwa wakati serikali inajaribu kukabiliana na hali hiyo, “watu wengi kwenye jamii zinazowahifadhi wanaonyesha ukarimu mkubwa na mashirika ya misaada ya kibinadamu inawaunga mkono lakini msaada wa jamii ya kimatifa unahitajika.

Kufikia sasa ombi la msaada wa kibinadamu kwa Ethiopia linahitaji dola bilioni 1.3 limefadhiliwa kwa asilimia 51 tu na fedha zaidi zinahitajika kwa jili ya misaada ya lishe, afya, makazi, uhifadhi, elimu na mahitaji mengine.

Bwana Lowcock pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu usalama wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu kufuatia kuuawa kwa wafanyakazi wawili kutoka mashirika yanayotambulika yasiyo ya kiserikali eneo la Gambella wiki iliyopita akisema, “tunalaani shambulio hilo la kikatili na tunajadili athari na wadau wote.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud