Kila sekunde 40 mtu mmoja anakufa kwa kujiua-WHO

9 Septemba 2019

Idadi ya nchi zenye mikakati ya kitaifa ya kuzuia watu kujiua imeongezeka katika kipindi cha miaka mitano tangu shirika la afya duniani WHO lilipotoa ripoti ya kwanza ya dunia kuhusu visa vya kujiua, limesema shirika la WHO kupitia ukurasa wake wa tovuti kuelekea siku ya kimataifa ya kuzuia kujiua inayoadhimishwa kila mwaka mwezi Septemba tarehe 10.

Hata hivyo WHO imesema nchi ambazo zina mikakati, ni 38 na bado ni chache hivyo serikali zinatakiwa kuhakikisha zinaanzisha mikakati hiyo.

“Pamoja na hatua zilizopigwa, mtu mmoja bado anafariki dunia kwa kujiua kila sekunde 40,” amesema Mkurugenzi mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus akiongeza kuwa, “kila kifo ni janga kwa familia, marafiki na jamaa. Wakati huohuo kujiua kunazuilika. Tunatoa wito kwa nchi zote kuingiza mikakati ya kuzuia kujiua katika programu za kitaifa za afya na elimu kwa namna endelevu.”

Idadi ya visa vya kujiua iko juu katika nchi za kipato cha juu; n ani sababu ya pili inayosababisha vifo miongoni mwa vijana

Kiwango cha wastani cha kujiua ulimwenguni kwa mwaka 2016 kilikuwa ni watu 10.5 kwa kila watu 100,000. Hata hivyo viwango vilikuwa na tofauti kubwa, kati ya nchi na nchi kutoka kwa watu watano wanaojiua kati ya watu 100,000 hadi kufikia zaidi ya watu 30 kwa watu 100,000. Wakati asilimia 79 ya visa vya kujiua kote duniani vilitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, huku nchi za kipato cha juu zilikuwa na viwango vya juu kwa watu 11.5 kati ya watu 100,000.

Ni nani kati ya wanawake na wanaume hujiua zaidi?

Ripoti ya WHO pia imeendelea kueleza kuwa kwa viwango vya wastani vya kujiua ulimwenguni kwa mwaka 2016 visa vya kujiua kwa wanaume wa nchi zilizoendelea ilikuwa ni mara tatu ya wanawake katika nchi hizo, huku ikiwa tofauti katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ambapo viwango vya visa kati ya wanawake na wanaume vinalingana.

Kujiua kulikuwa sababu ya pili baada ya ajali za barabarani inayosababisha vifo miongoni mwa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 29. Miongoni mwa barubaru wa umri wa miaka 15 hadi 19, kujiua ilikuwa sababu ya pili ya vifo miongoni mwa wasichana ikitanguliwa na sababu za vifo zinazosababishwa na masuala ya ujauzito, na sababu ya tatu inayosababisha vifo miongoni mwa wavulana baada ya ajali za barabarani na ugomvi miongoni mwao.

Nini kifanyike?

Njia ambayo imezoeleka zaidi kwa watu kujitoa uhai ni kujinyong’a, kunywa sumu ya kuulia wadudu na matumizi ya silaha. Njia ambazo zimeonesha kusaidia kupunguza visa vya kujiua ni pamoja na kuzuia kuweza kufikia vitu vya kutumia kujiua, kuelimisha vyombo vya habari kuhusu namna ya kuripoti matukio ya kujiua, kufanya programu miongoni mwa vijana katika kujenga stadi zinazowawezesha kukabiliana na msongo wa mawazo katika maisha, utambuzi wa mapema, pia jinsi ya kuwafuatilia watu walioko hatarini kujiua.

Ripoti ya WHO iliyotolewa hii leo pia imeonesha kuwa udhibiti wa manunuzi ya sumu za kuulia wadudu unasaidia sana kupunguza uwezekanoi wa watu kujiua ikitolewa mifano ya nchi kama Sri Lanka ambako visa vya kujiua vilishuka kwa asilimia 70 na inakadiriwa maisha ya watu 93,000 waliokolewa kati yam waka 1995 na 2015.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud