Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa UN-Habitat wafungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa pwani ya Kenya, Mombasa

Wanakikundi wa kundi la wakazi wa mtaa duni wa Majengo katika pwani ya Kenya ambao wanaduka za kuuza maji kwa ajili ya kujipatia kipato. (Agosti 2018)
© UN-Habitat/Kirsten Milhahn
Wanakikundi wa kundi la wakazi wa mtaa duni wa Majengo katika pwani ya Kenya ambao wanaduka za kuuza maji kwa ajili ya kujipatia kipato. (Agosti 2018)

Mradi wa UN-Habitat wafungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa pwani ya Kenya, Mombasa

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la makazi la Umoja wa Mataifa, UN-Habitat kwa kushirikian na serikali ya Kenya na wadau wametekeleza mradi wa kuimarisha makazi ya vitongoji duni kama sehemu ya mpango wa ukarabati wa jaribio wa nyumba za mabanda na kuwa makazi bora kwenye kaunti ya Mombasa.

Mradi huo ambao uliasisiwa mwaka 2014 umetekelezwa mtaa duni wa majengo nje ya Mtwapa kaskazini mwa pwani ya Kenya kaunti ya Mombasa na tayari umeanza kuzaa matunda kwani wenyeji wamefungua biashara akiwemo mkazi wa Majengo, Mathilda Chonga ambaye ni mmoja wa wanakikundi cha wajane 20 na amefungua biashara ya kuuza maji.

Bi. Chonga huku akitazama nje ya duka lake alfajiri anasema, "wateja wa kwanza hujitokeza muda mfupi baada ya saa 12 alfhajiri wakiwa na ndoo za maji mikononi mwao, tayari wanaanza kupanga foleni wachote maji safi ya kunywa."

Mradi huo wa maji ni wa gharama ya chini ambapo Bi. Chonga anasema, “kwa kweli, maji sio ya bure," Chongo anafafanua wakati anakusanya shilingi tatu za Kenya kwa lita 20 ambayo ni sawa na dola 0.03 za Marekani kutoka kwa mteja, akiongeza kwamba "lakini hii ni bei rahisi sana kuliko kawaida." 

Bi. Chonga ni mama wa watoto watatu na tangu aanze kupata mapato yake kutoka mauzo ya maji, ana pesa za kutosha kulipa ada za shule, vitabu na hata peremende chache kwa watoto.

Majengo na Mzambarauni, maeneo mawili ya makazi ya nje ya Mtwapa, yapo katika mchakato wa kubadilishwa kutoka miji yenye watu wengi ambayo ina makazi duni - kuwa vitongoji ambavyo vinakidhi miongozo na mahitaji.

 Mpango huo mpya utampa kila mkazi njia ya kupata maji safi ya kunywa huduma za kujisafi na pia ukarabati wa barabara za kutosha na kuwapa sehemu salama za kuishi. UN-Habitat inafanya kazi kwa kuwashirikisha pia wanajamii.

Mmoja wa wanajamii ambao wanashiriki katika kufanikisha mradi ni Albert Njama ambaye anaratibu mipango ya jamii, yeye ni amezaliwa na kulelewa Majengo  huku akisimulia hali ilivyo kuwa hapo awali akisema "Kulikuwa na nyumba chache za matope. Lakini kwa matarajio ya kupata kazi huku Mombasa, idadi inaongezeka ya watu kutoka maeneo mengine ambao wamehamia hapa kwa miongo mingi. Wakazi walichukua ndugu zao na marafiki. Ambapo nafasi iliruhusiwa, kulikuwa na ujenzi. Bila miundombinu, bila kupanga. Wakati fulani, idadi ya watu ilikuwa kubwa sana."

Moja ya changamoto zilizokwamisha maendeleo katika maeneo hayo ni kwamba wakazi hawana vyeti vya umiliki licha ya kwamba ni wakazi wa sehemu hiyo. Bwana Njama anaongeza "tunahitaji barabara zinazoweza kufikiwa na magari, magari ya wagonjwa na malori ya takataka. Tunahitaji taa za kuangaza barabarani, njia za kwa wasafiri wa miguu na barabara za maji taka."

Kwa sasa majadiliano yanaendelea na serikali ya Kenya kutoa hati miliki za ardhi kwa watu wa Majengo na Mzambarauni. 

"Hiyo ni hatua ya kufana kwa sisi sote," Njama anahitimisha akisema kuwa "ni kwa haki ya umiliki tu kwamba wenyeji wangehimizwa vya kutosha kufanya uwekezaji wa muda mrefu. "Hata hivyo, tunaweza tu kukuza zaidi ikiwa tunajua tunaruhusiwa kuishi hapa."