UNICEF yatandaza mabegi ya watoto kama makaburi ikitaka ulinzi zaidi wa watoto kwenye maeneo ya vita

Mabegi ya shule ya watoto yakiwa yametandazwa kama mfano wa makaburi kwenye viwanja vya makao makuu ya UN jijini New  York, Marekani kuashiria watoto waliokufa kwenye maeneo ya mizozo mwaka 2018.
© UNICEF/Farber/Getty
Mabegi ya shule ya watoto yakiwa yametandazwa kama mfano wa makaburi kwenye viwanja vya makao makuu ya UN jijini New York, Marekani kuashiria watoto waliokufa kwenye maeneo ya mizozo mwaka 2018.

UNICEF yatandaza mabegi ya watoto kama makaburi ikitaka ulinzi zaidi wa watoto kwenye maeneo ya vita

Amani na Usalama

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetandaza mabegi 3,758 ya mgongoni yanayotumiwa na watoto wa shule kuonyesha madhara ya vita kwa watoto kwa mwaka 2018.
 

Mabegi hayo yamepangwa kwa mfano wa makaburi ambapo kila begi moja linaashiria mtoto aliyepoteza  maisha kwenye maeneo yenye vita.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa jijini New York, Marekani imesema maonyesho hayo yatakuwepo hadi tarehe 10 mwezi Septemba mwaka huu ni ujumbe kwa viongozi wa dunia maeneo mbalimbali ulimwenguni wakati huu ambapo watoto wanarejea shuleni siku chache kabla ya kuanza kwa mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

UNICEF imesema pindi maonyesho hayo yatakapomalizika, mabegi hayo yatachukuliwa kuendeleza safari ya kusaidia elimu kwa watoto.

 “Mabegi ya mgongoni yanayotolewa na UNICEF kwa watoto yamekuwa kila wakati ishara ya matumaini na uwezo ambao mtoto anaweza kufikia pindi akipatiwa msaada,” amesema Henrietta Fore, Mkurgenzi Mtendaji wa UNICEF.

Amesema kuwa siku chache zijazo, viongozi wa dunia watakusanyika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kusherehekea miaka 30 tangu kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC na hivyo maonyesho hayo ya mabegi lazima yawakumbushe kuwa mustakabali wa watoto uko hatarini.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya watoto 12,000 waliuawa au kulemazwa kwenye maeneo ya mizozo mwaka jana pekee wa 2018, na hivyo kufanya kuwa idadi kubwa zaidi tangu Umoja wa Mataifa uanze kufuatilia takwimu hizo.

UNICEF inasema kwenye maeneo ya mizozo kama vile Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Somalia, Sudan Kusini, Syria na Yemen watoto wanalipa gharama kubwa ya vita.