Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rejesha ardhi katika ubora wake ili kuiokoa dunia na kukuza uchumi- Ibrahim Thiaw

Mabadiliko ya tabianchi na matumizi mabaya ya ardhi yamechangia katika kusababisha jangwa kwa mfano katika eneo la kaskazini mashariki mwa Cameroon (Januari 2019)
UN News/Daniel Dickinson
Mabadiliko ya tabianchi na matumizi mabaya ya ardhi yamechangia katika kusababisha jangwa kwa mfano katika eneo la kaskazini mashariki mwa Cameroon (Januari 2019)

Rejesha ardhi katika ubora wake ili kuiokoa dunia na kukuza uchumi- Ibrahim Thiaw

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa 14 wa nchi wanachama wa mkataba wa kuzuia kuenea kwa jangwa, UNCCD ukiendelea huko  New Delhi, India, Katibu Mtendaji wa mkataba huo Ibrahim Thiaw amesema  dunia sasa inatakiwa kuwekeza katika urejeshaji wa ardhi katika ubora kama njia mojawapo ya kuboresha ustawi wa maisha, kupunguza hatari za mabadiliko ya tabianchi  na kupunguza hatarizinazoweza kuyumbisha uchumi.

Bwana Thiaw alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani kwa njia ya video kutoka New Delhi ambako anashiriki mkutano  huo COP14, ulioanza tarehe 2 hadi13 ya mwezi huu wa Septemba ukiwa na kaulimbiu “kuwekeza katika ardhi,kufungua fursa”.

“Ardhi inatupatia asilimia 99.7 ya nguvu tunazopata na maji tunayokunywa. Ardhi ni mchangiaji mkubwa katika uchumi wetu. Pia ina uhusiano na afya yetu. Dhoruba za mchanga na vumbi ni visababishi vya matatizo katika maeneo mengi ya dunia hususani yanayohusiana na magonjwa kama pumu,” amesisitiza Bwana Thiaw.

Kwa upande wa ukame, Thiaw amesema katika mwaka uliopita yaaani 2018, nchi 25 ziliingia katika dharura ya ukame. Zaidi ya nchi 70 zimeathirika na ukame nan chi za namna hiyo zinahangaika na uhaba wa chakula.

Tweet URL

 

Aidha ameeleza kuwa kuna uhusiano kati ya amani na usalama, “hali katika eneo la Sahel ni mchanganyiko wa sababu nyingi zikiwemo kushindania ardhi na maji. Watu wengi walioathirika wako barani Asia na eneo lililoathirika zaidi ni Afrika.”

Akijibu maswali ya wanahabari, Bwana Thiaw amesema mkutano unaoendelea India unategemewa kukubaliana kuhusu maamuzi 30 katika mpango wa kuhakikisha malengo yam waka 2018 hadi 2030 yanafikiwa.

Pande zote zinazoshiriki zitapitisha makubaliano kuhusu udhibiti wa mmomonyoko wa udongo ambayo yayawasilishwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi mnamo tarehe 23 Septemba mwaka huu wa 2019 ambao utaeleza kuwa uboreshaji wa ardhi ni sehemu moja ya suluhisho katika kupambana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.