Kifo cha Mugabe, UN yatuma rambirambi na kusema itaendelea kusimama kidete na taifa hilo

6 Septemba 2019

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe amefariki dunia hii leo huko Singapore, alikuwa na umri wa miaka 95.

Kufuatia taarifa za kifo chake, msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari hii leo amesema Katibu Mkuu wa Umoja huo António Guterres atatuma barua kwa serikali ya Zimbabwe kuelezea rambirambi zake kwa serikali, wananchi na familia yake kufuatia msiba huo.

Ametambua mchango wa Hayati Mugabe katika kusaka uhuru wa Zimbabwe na vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, mambo ambayo amesema yatambukwa zaidi kuwa ni mchango wake.

Bwana Dujarric alipoulizwa na waandishi wa habari ni vipie anaweza kumuelezea hayati Mugabe na uhusiano wake na viongozi mbalimbali wa Umoja wa Mataifa, amesema kwamba, “Rais Mugabe mara nyingi alifika kwenye Baraza Kuu ambapo alikuwa na vikao na makatibu wakuu.”

Ameongeza kuwa, “nadhani kutokana na mtazamo wetu, Rais Mugabe amekuwa na mchango mkubwa wakati alipokuwa mwenyekiti wa Jumuiya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, na kama nilivyosema mara nyingi alikuwa mshiriki wa mikutano na vikao hapa Umoja wa Mataifa.”

Bwana Dujarric amesema Umoja wa Mataifa bado umejizatiti kwa dhati kusaidia Zimbabwe katika juhudi zake za kuendeleza utulivu jumuishi, maendeleo endelevu, utawala wa kidemokrasia na haki za binadamu.

Mugabe, alikuwa kiongozi wa kwanza wa Zimbabwe huru mwaka 1980 akichaguliwa kuwa Waziri Mkuu baada ya utawala wa kidhalimu na kisha kubadili mfumo wa serikali na kuwa Rais wa taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Aliondoka madarakani mwezi Novemba mwaka 2017 kufuatia mapinduzi ya kijeshi na kufuatiwa na uchaguzi mwaka 2018 uliomweka madarakani rais wa sasa Emmerson Mnangagwa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii