Mwanamke mvenezuela aweka rehani maisha yake ili kunusuru wanae wanne

6 Septemba 2019

Mamia ya maelfu ya raia wa Venezuela wanaendelea kuweka maisha yao rehani na kufanya safari za hatari ili kukwepa hali ngumu ya maisha nchini mwao na kukimbilia nchini jirani ambako shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR linashirikiana na nchi mwenyeji kuwasaidia.

 

Nats..

Kila uchao misafara ya wavenezuela kukimbilia nchi jirani inashuhudiwa na miongoni mwao ni Isbel Bolivar mwenye umri wa miaka 30 ambaye yeye alihisi hana namna ila kuondoka Venezuela kwa ajili ya watoto wake wanne.

Mwanamke huyu anayehudumia familia pekee yake, alianza nao safari ya hatari kwa miguu kwenda Colombia.

Colombia sasa inahudumia wakimbizi na wahamiaji milioni 1.4 kutoka Venezuela waliokimbia machungu kama anavyosimulia Isbel.

(Sauti ya Isbel)

"Niliona watoto wangu hawachezi tena, hawachori picha na walianza kuniambia, mama unga umeisha, mchele umeisha. Mama huu hapa msaada. Walishinda saa 24 bila chakula. Mwanangu Jeremías alilazwa hospitalini kwa sababu ya utapiamlo. Alikuwa na uzito wa kilo 7 akiwa na umri wa miaka 3. Alikuwa anakufa. "

Wengi hawawezi kusafiri kwa basi au gari, na kwa hivyo hutembea kutoka mpakani hadi miji ya Colombia kama vile Bucaramanga, Medellin, Cartagena, Cali na Bogota.

 Wengine hata hutembea mbali hadi Ecuador, Peru, au Chile, maelfu ya kilometa.

Kama wakazi wengi wa Venezuela, Isbel hakuweza kumudu usafiri alisafiri muda mrefu akipanda na kushuka milima

 (Sauti ya Isbel)

 “Tuliogopa sana kwa sababu hatukuwa tumezoea”

Hatimaye Isbel na watoto wake wanne walitembea hadi jimbo la Carabobo nchini Venezuela, na kuingia Medellin nchini Colombia ambako wanaishi katika makazi ya manispaa inayopata msaada kupitia UNHCR.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter