Harakati za usaidizi visiwa vya Bahama zaendelea, idadi ya waliokufa ikifikia 23

5 Septemba 2019

Tathmini za awali zikidokeza kuwa kimbunga Dorian kimesababisha watu 76,000 kwenye maeneo mbalimbali ya visiwa vya Bahama , kuhitaji misaada ya dharura, shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP linaandaa kupeleka shehena ya tani 8 ya vyakula ambavyo viko tayari kuliwa ikiwa ni sehemu ya msaada wake wenye thamani ya dola milioni 5.4.

Kupitia taarifa aliyotoa mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa WFP Hervé Verhoosel amesema kuwa tayari timu ya shirika hilo iko Nassau, mji mkuu wa Bahama ikifanya tathmini ya kina ya uharibifu na kubaini wale walio na mahitaji zaidi.

Taarifa za vyombo vya habari zinasema kuwa, hadi leo mchana kwa saa za visiwa vya Bahama, watu 23 wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na kimbunga hicho, na maafisa wana hofu kuwa idadi inaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa wakati huu ambapo harakati za kusaka watu na uokozi zikiendelea.

Bwana Verhoosel amesema kuwa WFP hivi sasa inashirikiana na mamlaka ya usimamizi wa majanga ya visiwa vya Karibea, CDEMA pamoja na wadau, “kutambua mahitaji ya haraka zaidi na kupeleka msaada wa haraka kama vile vyakula vifaa vya mawasiliano na miundombinu.”

Tayari ndege inaandaliwa kutoka kituo kikuu cha Umoja wa Mataifa huko Panama ikiwa na vifaa vya uhifadhi, majokofu, jenereta na ofisi mbili zitajengwa kwenye kisiwa kikuu cha Bahama.

U.S. Coast Guard District 7
Madhara kutokana na kimbunga Dorrain ni dhahiri eneo la Treasure Cay, Bahamas walinda bahari kutoka Marekani wanashirikiana na vikosi Bahama katika kutafuta na kuokoa watu.

Halikadhalika WFP inapeleka vifaa vya setilaili ili kurahisisha mtandao wa mawasiliano kwa wahudumu wa shughuli za dharura kwenye visiwa hivyo vya Bahama.

Msemaji huyo ameeleza kuwa timu za kutathmini hali halisi zilifanya tathmini ya awali kwa njia ya anga siku ya jumatano kwa lengo la kuweza kufika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Ameongeza kuwa hivi sasa WFP imetenga dola milioni 5.4 kama sehemu ya fungu lake la miezi mitatu la usaidizi kwa sababu ya hali halisi visiwani humo kuwa mbaya.

Fedha hizo zitasaidia watu 39,000 kwa awamu ya kwanza, ambapo WFP itajikita kwenye kusambaza hadi tani 85 za vyakula vilivyo tayari kuliwa kwa watu walioathirika zaidi.

Taarifa hizi za WFP zinakuja siku moja baada ya Mkuu wa misaada ya dharura kwenye UN, OCHA Mark Lowcock kutembelea visiwa vya Bahama siku ya Jumatano na kutangaza kuwa ofisi yake itatoa dola milioni moja kutoka mfuko wa dharura, CERF ili kusaidia harakati za usaidizi nchini humo ambazo zinaongozwa na serikali ya Bahama.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud