Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Familia nchini Syria bado zinahangaika kuweza kuishi pamoja na mvua kuboresha mavuno

Familia ya wakulima wakivuna mahindi vijijini Aleppo Syria
WFP/Marwa Awad
Familia ya wakulima wakivuna mahindi vijijini Aleppo Syria

Familia nchini Syria bado zinahangaika kuweza kuishi pamoja na mvua kuboresha mavuno

Msaada wa Kibinadamu

Viwango vya kutosha vya mvua katika maeneo ya kilimo ya Syria pamoja na hali nzuri kiasi ya usalama, vimeboresha mavuno ikilinganishwa na mwaka jana lakini bei kubwa za vyakula  bado zinaweka ugumu kwa wasyria wengi, inasema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya tathmini ya usalama wa mazao na chakula CFSAM iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO na mpango wa chakula WFP, uzalishaji wa ngano unakadiriwa kuwa tani milioni 2.2 ikilinganishwa na kiwango cha chini cha mwaka jana cha tani milioni 1.2. Hata hivyo uzalishaji wa mwaka huu haujafikia wastani wat ani milioni 4.1 za kabla ya mgogoro yaani kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2011.

Makadirio ya uzalishaji wa shayiri ni tani milioni 2, mara tano zaidi ya ya uzalishaji wa mwaka jana wa 2018 na zaidi ya asilimia 150 juu ya asilimia ya viwango vya uzalishaji vilivyofikiwa kabla ya mgogoro.

Hata hivyo, bei za vyakula zimekuwa zikiongezeka kwa zaidi ya miezi 12 hadi 14 iliyopita kutokana na kuongezeka kwa bei za nishati na kuendelea kuporomoka kwa paundi ya Syria katika soko lisilo rasmi.

Aidha uhaba wa chakula unasalia kuwa changamoto kutokana na chuki inayoendelea, kuendelea kuhama makazi na ongezeko la wakimbizi wanaorejea.

Mwakilishi wa FAO nchini Syria, Mike Robson anasema, “Labda kuwe na ongezeko la usaidizi katika ustawi wa kilimo, hususani kwa familia za Wasyria ambao wako katika hali mbaya, utegemezi katika msaada wa chakula utabaki.”

Naye Cainne Fleischer, mkurugenzi wa WFP nchini Syria amesema, “baada ya miaka tisa ya janga, watu wa Syria wakiwemo wale wanaorejea kwenye vijiji vyao wanaendelea kukumbana na changamoto kubwa. Wengi wanashindwa kuwalisha na kuwasomesha watoto wao. WFP inaendelea kuhakikisha inasambaza msaada ambao unasawasaidia kuishi na hatimaye kujenga upya maisha yao.”

Takribani watu milioni 6.5 nchini Syria wanakadiriwa kuwa katika hali ya kukosa chakula na wanahitaji msaada. Pia watu milioni 2.5 wako hatarini kuingia katika hali ya kukosa uhakika wa chakula.

Hivi sasa WFP inatoa msaada wa chakula kwa zaidi ya watu milioni 4 kila mwezi katika majimbo 14 ya Syria yakiwemo maeneo yaliyoathirika na mgogoro kama vile kaskazini magharibi mwa nchi.