Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Melissa Fleming aanza jukumu lake la kuongoza Idara ya Mawasiliano UN

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kulia) katika picha ya pamoja na Melissa Fleming, Mkuu mpya wa Idara ya Mawasiliano UN. (04 Septemba 2019)
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kulia) katika picha ya pamoja na Melissa Fleming, Mkuu mpya wa Idara ya Mawasiliano UN. (04 Septemba 2019)

Melissa Fleming aanza jukumu lake la kuongoza Idara ya Mawasiliano UN

Masuala ya UM

Mkuu mpya wa Idara ya mawasiliano ya Umoja wa Mataifa, DGC, Melissa Fleming kutoka Marekani, leo ameanza rasmi jukumu lake la kuongoza idara hiyo.

Bi. Fleming ambaye amekuwa msemaji wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2009, anachukua nafasi ya Alison Smale wa Uingereza ambaye aliongoza idara hiyo kwa miaka miwili.

Mkuu huyo mpya wa DGC ameanza jukumu hilo rasmi hii leo baada ya kuapishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwenye makao makuu ya chombo hicho jijini New York Marekani.

Tukio hilo la leo lilishuhudia pia kuapishwa kwa wakuu wengine wa Idara za Umoja wa Mataifa ambao ni Catherine Pollard wa Guyana ambaye atawajibika na Idara ya Mkakati, Sera na Usimamizi ilihali Movels Abelian kutoka Armenia yeye atasimamia masuala ya Baraza Kuu na usimamizi wa mikutano.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kulia) na wakuu watatu wapya wa Idara za UN aliowaapisha hii leo 04 Septemba 2019
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kulia) na wakuu watatu wapya wa Idara za UN aliowaapisha hii leo 04 Septemba 2019

Uzoefu

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa, Bi. Fleming ana ujuzi wa miaka 25 katika masuala mkakati wa dira, ubunifu kwenye usimamizi na utaalamu wa mawasiliano katika mashirika ya kimataifa.

Amefanya kazi katika nyanja mbalimbali kuanzia haki za binadamu, usaidizi wa kibinadamu, uzuiaji wa mizozo, ujenzi wa amani, uhuru wa vyombo vya habari na uzuiaji kuenea kwa nyuklia pamoja na ulinzi na usalama.

Akiwa mkuu wa mawasiliano UNHCR, Bi. Fleming ameendesha kampeni za mashinani, matumizi ya mitandao ya kijamii, huduma za kusambaza habari kwa njia mbalimbali zikilenga vyombo vya habari, wahusani, umma, na wakimbizi wenyewe.

Uandishi wa Habari

Fleming alijunga na UNHCR baada ya kufanya kazi na shirika la nishati ya atomiki duniani, IAEA, ambako kwa miaka 8 alkuwa msemaji wa chombo hicho. Kabla ya kufanya kazi IAEA, allikuwa mkuu wa mawasiliano na vyombo vya habari kwenye shrike la usalama na ushirikiano Ulaya.

Kwa kipindi cha Oktoba 2016 hadi 2017 alikuwa kwenye timu ya mpito ya Katibu Mkuu wa UN.

Aliwahi pia kuwa mtaalamu wa mahusiano ya umma kwenye Radio Free Europe/ Radio Liberty jijini Munich, Ujerumani ambako alianza kazi yake ya uandishi wa habari.

Bi. Fleming ana shahada ya pili ya uandishi wa habari kutoka Chuo cha mawasiliano cha Chuo Kikuu cha Boston na shahada ya kwanza ya masomo ya kijerumani kutoka Chuo cha Oberlin.