Nina mashaka na hali ya waathirika wa kimbunga Dorian-Antonio Guterres

4 Septemba 2019

Kufuatia hali mbaya iliyosababishwa na kimbunga Dorian kaskazini mwa visiwa vya Bahama, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anaendelea kuwa na wasiwasi kuhusu maelfu ya watu walioathirika katika kisiwa cha Grand Bahama na Abaco, imeeleza taarifa yake aliyoitoa hii leo jumatano kupitia kwa msemaji wake.

“Katibu Mkuu anatuma salamu za rambirambi kwa familia za wale waliopoteza maisha katika janga na anawatakia kupona haraka wale waliojeruhiwa.” Imesema taarifa.

Taarifa hiyo imeeleza pia kuwa mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa masuala ya kibinadamu, OCHA, Mark Lowcock  atakuwa katika visiwa vya Bahama leo hii. Katika mji mkuu Nassau, Bwana Lowcock atakutana na Waziri mkuu wa visiwa hivyo Hubert Minnis kujadili msaada wa Umoja wa Mataifa na kuelezea kuungana mkono kwa Umoja wa Mataifa na wat una serikali ya visiwa vya Bahama.

“Umoja wa mataifa unazisaidia juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali katika kuokoa na kutoa misaada n ani sehemu ya vikosi vya kufanya tathmini ambavyo vimepangwa kuingia hii leo katika maeneo yaliyoathirika. Watu waliopoteza kila kitu wanahitaji malazi, maji safi na salama ya kunywa, chakula na dawa.” Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imefafanua.

Wakati huo huo Katibu Mkuu Guterres ametoa wito kwa wafadhili kutoa fedha kwa ajili ya misaada ya kibinadamu na juhudi za kuirejesha hali katika mazingira ya kawaida mara tu mahitaji yatakapokuwa yamefahamika.

Kimbunga Dorian kimeendelea kuvitikisa visiwa vya Bahama tangu jumamosi na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa misaada ya kibinadamu OCHA, hapo jana imesema kuwa kasi ya upepo wa kimbunga doriani ilifikia maili 157 kwa saa na zaidi kisha kuyapiga maeneo ya Elbow Cay katika visiwa vya Abaco vyenye wakazi 17,200 na kimeendelea kubaki juu ya kisiwa cha Grand Bahama, kaskazini mwa mkusanyiko wa visiwa vya Bahama ambako kunakadiriwa kuwa na wakazi 51,000. Hadi kufikia jana jumanne, mamlaka nchini humo zilikuwa zimethibitisha watu watano kupoteza maisha huku nyumba zikiezuliwa na majengo mengi mengine kusambaratishwa. 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud