Kuna hali ya hofu na vitisho nchini Burundi- COIB

4 Septemba 2019

Ikiwa imesalia chini ya mwaka mmoja kuelekea kufanyika uchaguzi wa rais,wabunge na serikali za mitaa nchini Burundi mwakani 2020, kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuichunguza Burundi COIB imetoa ripoti yake hii leo mjini Geneva Uswisi na kusema kuwa kuwa kuna hali ya hofu na vitisho kwa watu wote ambao hawaonyeshi kukiunga mkono chama tawala cha CNDD-FDD. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Ripoti hiyo imesema bado tawi la vijana la chama hicho liitwalo Imbonerakure, usalama wa taifa, polisi pamoja na serikali za mitaa wameendelea kutekeleza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia wa Burundi tangu kulipozuka mgogoro mwaka 2015 na hadi hivi sasa haujatatutiliwa kiasi cha kuathiri kila kona ya Burundi.

Ripoti imeeleza jinsi  Imbonerakure wametekeleza mauaji, kutoweka kwa watu, ukamataji watu kiholela, kuwaweka watu kizuizini, vitendo vya kuwatesa na kuwatendea vibaya ikiwemo ubakaji dhidi ya wanaodaiwa kuwa wapinzani au hata wanachama wa vyama vya upinzani. Kamisheni, imeona kwamba vurugu hizi zinachochewa na hali ya kulindwa kwa watekelezaji wa matukio hayo nchini Burundi.

Mwenyekiti wa kamisheni hiyo Doudou Diene amewaambia waandishi wa habari kuwa hivi sasa ni hatari kubwa kuzungumza wazi kuikosoa Burundi. Akaongeza kuwa hata amani inayoonekana kuwepo inatokana na kuminywa kwa sauti za watu na hivyo utulivu uliopo unatokana na hofu.

Akijibu swali la wanahabari kuhusu rais wa Burundi anahusika vipi kuweka mazingira nchini mwake, mmoja wa wajumbe watatu wa kamisheni hiyo  Françoise Hampson amesema,“anawajibika kwa kila kitu kinachofanywa na viongozi wa ngazi za chini mitaani. Na kumekuwa na mabadiliko tangu mwaka 2016 ambapo vijana wa Imbonerakure wamekuwa wakifanya kazi na mamlaka za mitaa kwa mfano wakizunguka kukusanya michango kwa ajili ya uchaguzi. Na wanayafanya hayo kwa ruhusa ya mamlaka. Kwa hivyo kwa mazingira hayo, mkuu wan chi anawajibika kwa namna nchi inavyoendeshwa na kwa kuruhusu mwanya ambao Imbonerakure wanaweza kutekeleza. Anawajibika kwa namna hiyo.”

Kamisheni hii ndiyo chombo pekee huru cha kimataifa kinachochunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchni Burundi na watawasilisha ripoti yao kwa Baraza la haki za binadamu litakalokaa mwezi huu wa Septemba tarehe 17.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter