Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimevunjika moyo na mwelekeo wa haki za binadamu duniani - Bechelet

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet
UN News/Daniel Johnson
Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet

Nimevunjika moyo na mwelekeo wa haki za binadamu duniani - Bechelet

Haki za binadamu

 Mwaka mmoja baada ya kushika jukumu la ukamishna wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema hakutarajia kuwa itakuwa kazi rahisi, lakini amevunjwa moyo kutokana na mwelekeo wa haki za binadama hivi sasa. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

Bachelet akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo amesema ana hofu kubwa ya kwamba dunia hivi sasa imeungana zaidi kuliko wakati wowote ule kiasi kwamba athari za haki za binadamu kwenye eneo moja zinaweza kuwa na madhara makubwa kikanda au kimataifa.

Kamishna Mkuu Bachelet amesema“tumeshuhudia hili kwa jinsi watu wengi wanakimbia nchi zao kutokana na mizozo, ukosefu wa usalama, ukandamizaji wa kisiasa, majanga ya tabianchi na kushinda kulinda haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.”

Bi. Bachelet pia ametaja kushamiri kwa kauli za chuki, kibaguzi na chuki dhidi ya wageni akisema vinasambaa kwenye kiza cha mitandao ya intaneti na dhahiri kabisa kwenye mitandao ya kijamii.

Ameenda mbali akisema kuwa “katika kila ukanda wa dunia: Hong Kong,  Urusi, Papua ya Indonesia, eneo la Kashmir lililo chini ya India, Honduras na Zimbabwe- na bila shaka Yemen n a Syria tunaona vilio vya watu wakihaha wakitaka mazungumzo."

Bi. Bachele amesema kwa kiasi kikubwa, machungu hayo yana uhusiano na ukosefu wa usawa na matumizi yasiyo sahihi ya madaraka. Pindi watu wenye uwezo mbalimbali wanaporuhusiwa kuketi meza moja, kujadili kwa wazi jinsi ya kupata haki zao za kitamaduni, kisiasa, kijamii na kichumi katika mazingira salama, bila hofu ya kukandamizwa, bila uoga, hapo tu ndio tutakuwa na matumaini ya utulivu."

Amekumbusha kuwa ukiukwaji wa haki za binadamu ni suala linalopaswa kushughulikiwa na kila mtu kwa kuwa linaathiri kila upande kuanzia amani, usalama, uchumi na hubisha hodi kwenye kila kaya.

Hata hivyo cha kusikitisha amesema mipaka ya nchi inatumika kuzuia ufuatiliaji wa haki za binadamu na hata wao wenyewe ofisi ya haki za binadamu huzuia kufanya hivyo jambo linalomtia hofu  akisema kwamba, “mienendo hii miwili inayoenda pande tofauti inaonekana kutuondoa kwenye suluhu za kimataifa kwenda kwenye matatizo ya kimataifa. Nasihi nchi zishirikiane kutatua masuala ya haki za binadamu kwa njia ya pamoja ya ushirikiano.”