Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia yakabiliwa na kiwango kidogo cha mavuno ya nafaka

Katika eneo lililoathirika kwa ukame nchini Somalia, familia zinatelekeza makazi yao na kuelekea mijini au katika maeneo wanakoweza kupata usaidizi
© European Union 2017 (photographer: Anouk Delafortrie)
Katika eneo lililoathirika kwa ukame nchini Somalia, familia zinatelekeza makazi yao na kuelekea mijini au katika maeneo wanakoweza kupata usaidizi

Somalia yakabiliwa na kiwango kidogo cha mavuno ya nafaka

Tabianchi na mazingira

Mavuno ya nafaka nchini Somalia kwa mwaka huu wa 2019 yamekuwa ni kiwango cha chini zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu mwaka 2011, na hivyo kuliweka taifa hilo katika hali tete ya uhakika wa chakula.

Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, George Conway amesema hayo leo mjini Mogadishu, Somalia wakati wa mkutano na wanahabari uliofanyika kuwasilisha ripoti ya takwimu za mavuno baada ya msimu wa upanzi wa mwezi Aprili hadi Juni ujulikanao kama Gu nchini humo.

Sababu kuu ni mvua zisizo na mwelekeo wakati wa msimu huo sambamba na kiwango kidogo cha maji kwenye mito.

Takwimu hizo zilizokusanywa na kitengo cha uchambuzi wa uhakika wa chakula na lishe cha shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO na mtandao wa mfumo wa maonyo kuhusu tahadhari ya njaa, FEWNET, zinaonesha kuwa uzalishaji wa nafaka ulikuwa asilimia 70, ikiwa ni wastani wa chini kwenye maeneo ya kusini wakati wa kipindi husika cha Gu.

Ripoti inaonesha kuwa kupungua kwa mavuno kumesababisha kuongezeka kwa bei ya mtama wakati wa msimu huo wa Gu.

Kwa kuzingatia hali ya sasa, ripoti inasema kuwa, “bila usaidizi wa kibinadamu, takribani watu milioni 2.1 nchini Somalia watakabiliwa na njaa hadi mwezi Disemba mwaka huu, na hivyo kufanya idadi ya wasomali wasio na uhakika wa chakula ifikie milioni 6.3."

Akifafanua Bwana Conway amesema, “kwa ujumla mpango wa usaidizi wa kibinadamu kwa mwaka 2019 umechangiwa kwa chini ya asilimia 50 na tunahitaji ahadi zaidi kutoka kwa wafadhili na wadau wetu ili tuendelee na kiwango cha sasa cha usaidizi, kwa sababu tusipofanya hivyo kuna hatari ya idadi ya wenye uhitaji kuongezeka na hii itakuwa mbaya.”

Hali tete za tabianchi na kuenea kwa umaskini ni moja ya vichocheo vya mamilioni ya wasomali kutwama kwenye njaa ambapo Waziri wa masuala ya kibinadamu na usimamizi wa majanga, Hamza Said Hamza anasema kwamba, “tunatarajia mvua kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba. Tunaweza kuwa na mambo mawili. Mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko Somalia, kwa sababu unafahamu kuna mito.”

Naye Naibu Mwakilishi wa FAO nchini Somalia, Etienne Peterschmit amesema kuwa “jambo muhimu ni kutambua kuwa idadi kubwa ya wasio na uhakika wa chakula wanaishi vijijini kwa hiyo tunazungumzia kuwezesha watu wazalishe mazao na waweze kuishi kwenye maeneo hayo.”

Msimu ujao wa upanzi au Deyr wa kati ya mwezi Oktoba na Desemba unatarajiwa kuwa na kiwango kikubwa cha mvua ambazo maji yake yanatarajiwa kusababisha mafuriko kwenye mito ya Juba na Shabelle na hivyo kuharibu mazao.