Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kimbunga Dorian chaendelea kutishia maisha katika visiwa vya Bahamas, Umoja wa Mataifa watoa neno

Kimbunga Dorian kinavyoonekana kutoka katika kituo cha anga cha NASA hii leo Septemba 2, 2019
NASA
Kimbunga Dorian kinavyoonekana kutoka katika kituo cha anga cha NASA hii leo Septemba 2, 2019

Kimbunga Dorian chaendelea kutishia maisha katika visiwa vya Bahamas, Umoja wa Mataifa watoa neno

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake ameeleza kusikitishwa kwake na hali mbaya ya uharibifu uliosababishwa na kimbunga Dorian ambacho hivi sasa bado kinaendelea kupiga maeneo ya Bahamas.

Msemaji wa Katibu Mkuu Bwana Stephane Dujarric katika tarifa hiyo aliyoitoa leo jumatatu mjini New York Marekani, amesema Katibu Mkuu yuko pamoja na watu na serikali ya Bahamas katika hali waliyonayo hivi sasa.

“Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia juhudi zinazoongozwa na serikali kuokoa na kutoa misaada.” Imesema sehemu ya tarifa hiyo.

Tweet URL

 

Naye rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika kuwa, “tuko pamoja na watu wote walioathirika na uharibifu wa kimbunga Dorian. Tunaifuatilia kwa karibu hali na tunaisihi jumuiya ya kimataifa kuwa tayari kusaidia.”

Taarifa za awali za vyombo vya habari zinasema huenda kukawa na vifo kadhaa kutokana na kimbinga hicho kilichovipiga visiwa vya Bahamas na kikitarajiwa kusogea hadi katika pwani ya mashariki mwa Florida Marekani na maeneo mengine. Nyumba nyingi katika visiwa vya Bahamas zimeeziliwa na kimbunga hicho.