Umoja wa Mataifa hautawatelekeza watu wa DRC-Antonio Guterres

2 Septemba 2019

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo mara baada ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Kidemkorasia ya Congo Felix Tshisekedi mjini Kinshasa, amezungumza na wanahabari kuwaeleza kwa ufupi kuhusu mkutano wake na rais na masuala waliyoyajadili kuanzia usalama na mlipuko wa magonjwa.

Bwana Guterres ameanza kwa kuwaeleza wanahabari kuwa katika siku mbili alizokuwa jimboni Kivu Kaskazini, ameona kuwa kuna upepo wa matumaini unaovuma nchini DRC.

Aidha amewaeleza kuwa amekuwa na fursa ya kukutana na Rais Tshisekedi na kuzungumzia dhamira yao kuwa leo ni kuna tukio la kihistoria nchini Congo, hali ambayo inaweza kutegemea maendeleo ya taasisi za kidemokrasia, uwepo wa serikali inataka kuibadilisha nchi, lakini pia uwepo wa upande wa upinzani ambao pia wanachangia katika upande muhimu wa maisha ya kisiasa ya nchi, kuheshimu haki za binadamu na maono kwa mstakabali wa DRC.

"Nilikuwa Kivu Kaskazini na niliweza kuona ukubwa wa tishio la kundi la ADF na matendo yao ya kigaidi yasoiyovumilika dhidi ya watu wa Congo." Ameeleza Bwana Guterress kisha akaongeza, "tumekubaliana kuwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC MONUSCO wataimarisha uwezo wao kwa ajili ya hatua dhidi ya ADF na pia wataimarisha ushirikiano wao na vikosi vya Jamhuri ya kidemokrasia ya ili kushughulikia vema suala la usalama wa watu ambapo si tishio kwa watu wa DRC tu bali pia tishio la kimataifa."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia vyombo vya habari mjini Kinshasa DRC, Septemba 2, 2019
MONUSCO/Michael Ali
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia vyombo vya habari mjini Kinshasa DRC, Septemba 2, 2019

 

Bwana Guterres akijibu maswali ya wanahabari ameendelea kueleza, "tumekuwa na mjadala mzuri na rais wa Jamhuri hii  na nina uhakika ndani ya mpango mkakati wa MONUSCO, Baraza la usalama litaamua masuala kadhaa ambayo yanaweza kuboresha MONUSCO na ushirikiano wake na serikali ya DRC ili kuweka mazingira ambayo yataruhusu siku moja, MONUSCO kutokuwa muhimu tena hapa na kuwa uhusiano kati ya MONUSCO na Umoja wa Mataifa utakuwa wa kawaida ambapo watu wa Umoja wa Mataifa watafanya kazi na watu wa serikali kwa ajili ya ustawi wa watu wa DRC. Lakini kwa sasa bado tuko na DRC na niseme kwa uwazi kabisa; Umoja wa Mataifa hautawatelekeza watu wa DRC."

Kwa upande wa Ebola ameeleza kuwa ni muhimu sana kupambana na Ebola ingawa pia ameona kuwa mapambano hayo hayahusu Ebola pekee kwani kuna magonjwa mengine kama Surua, Maralia na kipindupindu.

Ameeleza namna alivyofurahi kukutana na manusura wa Ebola ambao walipatiwa matibabu kwa haraka na kupona, "kuna operesheni ya chanjo ya muhimu dhidi ya Ebola inayoendelea. Kuna vituo vya ukaguzi lakini pia vituo vya matibabu ambavyo nimevitembelea na sasa kuna tiba dhidi ya Ebola. Hayo ni mabadiliko makubwa."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa nchini humo DRC kwa ziara ya siku tatu tangu juzi jumamosi.

 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter