Siku ya pili ya ziara, Katibu Mkuu wa UN awapongeza walinda amani pamoja na wananchi wa DRC kwa ushujaa na kujitolea kwao

1 Septemba 2019

Katika siku ya pili ya ziara yake nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza heshima aliyonayo kwa wananchi wa DRC pamoja na kujitolea kwa walinda amani waliopoteza maisha wakiwahudumia wananchi.

Bwana Guterres ameyasema hayo akizungumza hii leo jumapili katika mkutano na vyombo vya habari katika mji wa Beni ambao ni kitovu cha mlipuko wa ugonjwa mkali wa Ebola ambapo amesema watu wa eneo hili pia wanakabiliwa na matatizo mengine mazito kama vile surua, malaria na ukosefu wa usalama.

Akiwahutubia wanahabari kwa lugha ya kifaransa Bwana Guterres amesema, “ni matumaini yangu kuwa uwepo wangu hapa leo unasisitiza tena uungaji wangu mkono kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO katika mapambano dhidi ya makundi yenye silaha ambao wanasambaza hofu na vifo. MONUSCO na wadau wake yaani vikosi vya ulinzi vya DRC, na polisi wa kitaifa wa DRC wanaendelea kufanya kazi pamoja kuleta amani na usalama katika ukanda huu.”

 

Katibu Mkuu huyo ameendelea mbele na kueleza salamu zake za rambirambi kwa familia na wapendwa wa waathirika wa vurugu na akatoa wito kwa makundi yote yenye silaha kwa haraka kusitisha mashambulizi yao kwa wananchi pamoja na vikosi vya usalama vilivyotumwa kuwalinda wananchi wa Congo, “walinda amani wamelipia gharama kubwa katika kulinda amani. Lakini hayo yanaimarisha lengo letu. Tutafanya kila tuwezalo kumaliza ukosefu wa amani katika eneo hili. Ni muhimu watu wa Beni wafahamu kuwa tunakisikia kilio cha mateso yao.”

Bwana Guterres ameongeza kuwa mfumo wa Umoja wa Mataifa umejizatiti kuzisaidia mamlaka za DRC, jamii na asasi za kiraia katika mapambano dhidi ya ukosekanaji wa usalama, na kuwa atalijadili suala hili pamoja na mamlaka za kitaifa katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa katika siku zijazo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud