Mradi wa kilimo kwa ajili ya amani, mkombozi wa wanawake na vijana CAR

3 Septemba 2019

Nchini Jamhuri ya Afrika ya kati CAR, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanawasaidia wanawake kwenye mji wa Birao jimbo la Vakaga, kujenga amani kwa njia bora zaidi, wakifanya kazi ya kilimo kulisha familia zao na kupata riziki. 

Ofisi ya shamba huko Birao linakusudia kuleta jamii pamoja wakati likiwasaidia kupata mbinu za mafunzo ya kilimo na njia ambazo pia ni pamoja na usimamizi wa fedha.

Pamoja na matokeo ya faida, jamii sasa imechukua umiliki wa mradi huu, kuendesha biashara ya shamba peke yao kwa kutumia stadi walizojifunza kutoka kwa kikosi cha maafisa wa Zambia kilichoko C.A.R.

Zara Hussein, anatoa shukrani kwa walinda amani,

(Sauti ya Zara Hussein)

"Wanatufundisha namna nzuri za kulima. Tumejumuishwa makabila tofauti tofauti na MINUSCA inatuonyesha jinsi ya kuishi na kufanya kazi pamoja kwa njia za kijamii. Tunataka amani."

Kilomita chache kutoka shamba hilo ni soko la wazi la Birao, wafanyabiashara wengi wanawake hukusanyika hapa mara moja kwa wiki kuuza bidhaa zao.

Soko hili limewezeshwa na ushiriki wa vikundi mbali mbali vya wanawake katika miradi ya maendeleo, mchango wao unathaminiwa, kwani wanasaidia kuingiza uhakika wa kiuchumi katika mkoa huo.

Vijana wengi wa eneo hilo wasio na ajira hawajaachwa. Kwa kufahamu ushawishi wa vikundi vyenye silaha kwa vijana wasio na kazi, MINUSCA inawalenga pia vijana walioko hatarini.

Zaidi ya vijana 700 wamelima shamba zaidi ya ekari 100 na wamepanda mihogo na matikiti.

Luteni Kanali Latson Ngosa, Kamanda wa Kikosi cha Zambia, MINUSCA, anasema,

(Sauti ya Luteni Kanali Latson Ngosa)

"Wahusika wa vurugu daima hukimbilia kwa vijana, ikiwa hawajashiriki kwa njia nzuri. Baada ya kukaa chini na wasimamizi wa shamba, tulidhani ni busara kwamba watu tunaowakumbatia kwa sasa ni vijana kwa kiwango cha kwamba mara tu tutakapowapa shughuli nyingi, hawapaswi kudanganywa kwa urahisi. Wakati huo huo, tuligundua kuwa kazi hazipatikani hapa, na tulidhani miradi kama hiyo inapaswa kuwezesha vijana kwa njia zenye tija na ambayo inapaswa kuwafanya wawe na shughuli nyingi ili kuepusha mtu yeyote kuidanganya na kwa kiwango fulani kuwawezesha kiuchumi."

Ukulima kwa ajili ya amani ni moja ya mipango ya ubunifu ya MINUSCA ya kudumisha utulivu wa kijamii na kiuchumi nchini humo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter