Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu Guterres na viongozi wengine waandamizi wa UN waonesha mshikamano na DR Congo katika ziara ya siku tatu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres baada ya kufika katika kambi ya MONUSCO Goma DRC (31 Agosti 2019)
UN /Martine Perret)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres baada ya kufika katika kambi ya MONUSCO Goma DRC (31 Agosti 2019)

Katibu Mkuu Guterres na viongozi wengine waandamizi wa UN waonesha mshikamano na DR Congo katika ziara ya siku tatu

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na viongozi wengine waandamizi wa Umoja wa Mataifa hii leo wameanza ziara ya siku tatu nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC ambako wananchi wanakabiliwa na ukosefu wa usalama na janga la afya linaloendelea ikiwemo Ebola ambayo imeshawaua watu 2000.

Bwana Guterres amewasili katika mji wa Goma ulioko katika mkoa wa Kivu Kaskazini ambako ndiko kitovu cha mlipuko wa Ebola. Huko Goma amepokelewa na mwakilishi wake maalumu nchini humo, Bi Lela Zerrougui kisha akakagua kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa na kuwashukuru kwa huduma yao na kujitolea kuweka maisha yao hatarini ili kuwalinda wananchi.

Tweet URL

 

Naye mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean Pierre Lacroix, ambaye ameielezea zaira hiyo ya viongozi wa juu kama fursa ya kusisitiza kuunga mkono juhudi za kuelekea kwenye amani na utulivu nchini DRC, ameungana na Bwana Guterres katika safari hiyo. Ameeleza kuwa mfumo wote wa Umoja wa Mataifa ikiwemo ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, wamejizatiti vilivyo kuitokomeza Ebola.

Pia wananchi nchini DRC wanakabiliwa na madhara mabaya ya magonjwa mengine kama surua na malaria, ambapo hayo mawili kwa pamoja yanaua watu wengi zaidi kuliko Ebola, amekumbusha Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya ulimwenguni Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus. Tedros ambaye ni sehemu ya wajumbe wa Umoja wa Mataifa walioko katika ziara hiyo amesema hii ndiyo maana uwekezaji katika mifumo ya afya kwa kuzingatia afya ya msingi ni muhimu ili kushughulikia mahitaji yote ya kiafya kwa njia kamilifu.

Katibu Mkuu Antonio Guterres akizungumza na uongozi wa MONUSCO. Kulia ni Leila Zerrougui na kushoto ni Jean-Pierre Lacroix
UN/Matine Perret
Katibu Mkuu Antonio Guterres akizungumza na uongozi wa MONUSCO. Kulia ni Leila Zerrougui na kushoto ni Jean-Pierre Lacroix

 

Akizungumza na wanahabari kwa lugha ya kifaransa, Bwana Guterres ameeleza kufurahishwa kwake na ustahimilivu wa watu wa DRC na akasisitiza ushirikiano wa Umoja wa Mataifa katika kupambana na ugaidi, siyo tu nchini DRC lkini kote barani Afrika na duniani kote.

Kwa upande wa hali mbaya ya Ebola, na masuala mengine makubwa ya afya kama vile surua, malaria na kipindupindu, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameahidi kuwa “Umoja wa Mataifa unasimama bega kwa bega mamlaka za DR Congo na watu wan chi hiyo ili kufanya kila tuliwezalo kukabiliana na changamoto hizi.”

Wakati wa ziara yake hii ya kwanza tangu alipoanza kuuongoza Umoja wa Mataifa mwezi Januari 2017, Bwana Guterres atakutana na viongozi wa ngazi za juu za serikali, wadau katika mchakato wa amani wa DRC, raia, poilisi na wanajeshi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Viongozi wengine alioambatana nao ni pamoja na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Maziwa makuu Michel Kafondo; Matshidiso Moeti ambaye ni Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika; Mike Ryan Mkurugenzi mtendaji wa programu ya dharura za afya ya WHO na Ibrahima Socé Fall, Mkurugenzi mkuu msaidizi wa huduma za dharura za WHO.