Kile kinachoendelea Syria lazima kibadilike, wananchi wamechoka- Pedersen

© UNICEF/Delil Souleiman
Mtoto akiwa kwenye kambi ya muda huko Ain Issa nchini Syria. (3 Juni 2019)
© UNICEF/Delil Souleiman

Kile kinachoendelea Syria lazima kibadilike, wananchi wamechoka- Pedersen

Amani na Usalama

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Geir Pedersen amesema kiwango cha ghasia na ukosefu wa utulivu nchini humo kinatia wasiwasi mkubwa huku idadi ya vifo ikiongozeka kila uchao na wakimbizi wa ndani nao ni mamilioni na hivyo mwelekeo huo lazima ubadilike.

Bwana Pedersen amesema hayo leo jijini New York, Marekani wakati akihutubia Baraza la Usalama lililokutana kujadili hali ya kisiasa na kibinadamu nchini Syria ambapo amesema kuwa “makumi ya maelfu ya raia wanashikiliwa au wamepotea Syria na taarifa zao hazielezwi huku eneo kubwa la taifa hilo likiwa limeganywa vipande vipande miongoni mwa makundi tofauti yanayopigana.”

MAPIGANO YAMESHAMIRI

Ametolea mfano eneo la Idlib, akisema kuwa mapigano yanaendelea bila kukoma akisisitiza kuwa mbinu za kukabiliana na ugaidi haziwezi kuweka hatarini raia milioni 3 ambao wana haki ya kulindwa chini ya sheria ya kibinadamu ya kimataifa. “Suluhu ya hali ilivyo sasa kwenye nchi hii linapasa kuwa la kisiasa,” amesisitiza.

Pedersen ameongeza kuwa mvutano kati ya Israel na Iran nao unazidi kutia wasiwasi hususan kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel kwenye viunga vya mji mkuu Damascus. “Nasihi pande zote ziheshimu uhuru wa Syria na bila shaka wa mataifa yote yaliyopo eneo hilo na kujizuia kufanya mashambulizi na uchochezi kwa vitendo na kauli.”

Hata hivyo mjumbe huyo maalum amesema licha ya mapigano hayo, hajakata tamaa na ameendelea na juhudi zake za kuhamasisha mashauriano baina ya wasyria katika kuandaa katiba mpya na kuendesha uchaguzi huru na wa haki chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Kuhusu kamati ya kikatiba, Bwana Pedersen amesema, “kuna uelewa mkubwa baina ya pande husika kuhusu; uwepo wa wenyeviti wawili wenza wenye mamlaka sawa, mmoja akichaguliwa na serikali na mwingine akichaguliwa na upinzani; uwezeshaji wa Umoja wa Mataifa ya wigo wa asilimia 75 ya upigaji kura huku kukiwepo na makubaliano; kuhusu chombo kikubwa chenye wajumbe 150 na chombo kidogo chenye wajumbe 45; kuhusu ahadi dhahiri ya hakikisho la usalama wa wajumbe wa kamati na familia zao.”

Mjumbe huyo amesisitiza kuwa tofauti zilizopo hivi sasa ni ndogo mno na ana matumaini kuwa Umoja wa Mataifa utakuwa kwenye nafasi ya kutangaza makubaliano kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Geir O. Pedersen, Mjumbe Maalum wa UN kwa Syria akihutubia Baraza la Usalama la UN leo kuhusu hali ya Syria. (29 Agosti 2019)
UN/Eskinder Debebe
Geir O. Pedersen, Mjumbe Maalum wa UN kwa Syria akihutubia Baraza la Usalama la UN leo kuhusu hali ya Syria. (29 Agosti 2019)

HALI YA KIBINADAMU

Wajumbe wa Baraza pia walijulishwa na Mkuu wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock kuwa zaidi ya raia 500 wameuawa na mamia wengine wamejeruhiwa tangu kuanza kwa mapigano mapya huko Kaskazini-Magharibi mwa Syria mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.

WHO na UNICEF waliripoti kuwa vituo 43 vya afya, vituo 87 vya elimu, vituo 29 vya maji na masoko 7 yameathiriwa kwa mapigano ya tangu mwezi Aprili,” amesema Lowcock akitoa wito kwa pande kinzani zihakikishe zinaheshimu sheria za kimataifa akiongeza kuwa “chombo cha uchunguzi kilichotangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kitachunguza matukio yaliyoharibu miundombinu ya huduma iliyopatiwa usaidizi na Umoja wa Mataifa huko kaskazini-magharibi wa Syria.”

Amesisitiza kuwa kanuni ziko bayana na pande husika nyakati zote zinapaswa kuzingatia kanuni za tahadhari zinapotekeleza matendo yao ili kuhakikisha zinalinda raia na miundombinu ya kiraia.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kutekeleza operesheni zake za kibinadamu na tayari umefikia watu milioni 6 mwaka huu pekee.

Hata hivyo amesema kuwa kadri uwezo wa kifedha unavyopungua kuliko mwaka 2018, nchi zilizotoa ahadi wakati wa mkutano wa Brussels zinapaswa kutekeleza ahadi zao.

MWAKILISHI WA SYRIA ADAI TAKWIMU ZA IDLIB SI ZA KWELI

Kwa upande wake Mwakilishi wa kudumu wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Bashar Jaafari amesema kuwa , “madai ya kwamba serikali ya Syria na washirika wake wanalenga hospitali, shule na miundombinu ya kiraia hayana msingi wowote,” akisisitiza kuwa vikosi vya Syria na vile vya Urusi vinalenga maeneo ya magaidi.

Amesema huko Idlib hakuna watu milioni 3, “idadi hii si ya kweli ni uongo. Idlib haina asilimia 20 ya wakazi wa Syria. Idlib ni jimbo dogo likilinganishwa na majimbo mengine Syria na idadi yake haizidi milioni 1.”

Balozi Jaafari amesema makubaliano kati ya Marekan ina Uturuki ya kuanzisha ukanda uitwao salama huko kaskazini-mashariki mwa Syria ni mbinu nyingine  ‘inayouacha uchi’ ubia kati ya Marekani na Uturuki katika uvamizi wao wa Syria na umedhihirisha hila ya mataifa hayo mawili ya kuingilia siasa za wengine.

Hata hivyo amesisitiza kuwa serikali ya Syria inaendelea kuazimia kushirikiana na mjumbe maalum wa Syria na kusisitiza kuwa uwepo wowote usio halali nchini Syria lazima ukome haraka ili mamlaka ya mjumbe huyo yaweze kufanikiwa.