Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Boti nyingine yazama Mediterania, UNHCR yarejelea wito wake wa kuokoa maisha

Picha ya maktaba katika bahari ya Mediterania, boti ikiwa imewabeba wahamaji na wanaotafuta hifadhi.
UNHCR/L.Boldrini
Picha ya maktaba katika bahari ya Mediterania, boti ikiwa imewabeba wahamaji na wanaotafuta hifadhi.

Boti nyingine yazama Mediterania, UNHCR yarejelea wito wake wa kuokoa maisha

Wahamiaji na Wakimbizi

Takribani watu 40 wanakadiriwa kufa kwa kuzama maji katika ufukwe wa Libya kufuatia kuzama kwa boti ya wahamiaji kuzama hii leo katika bahari ya Mediterania, taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa UNHCR imeeleza.

Tukio hili la kutisha limeifanya UNHCR kurejelea wito wake wa haraka wa kuchukua hatua za kuokoa maisha.

Manusura wapatao 60 wameokolewa na kuletwa ufukweni katika mji wa pwani wa Al-Khoms, takribani kilomita 100 mashariki mwa Tripoli. Shughuli ya uokozi iliyofanywa na walinzi wa pwani ya Libya pamoja na wavuvi imekuwa ikiendelea tangu asubuhi ya leo nab ado inaendelea.

“Hatutakiwi kuyakubali majanga haya kama yasiyoepukika,” amesema Vincent Cochetel, mwakilishi maalumu wa UNHCR katika eneo la Mediterania ya kati. “Masikitiko yanatakiwa sasa kuwa hatua zinazozuia kupotea kwa maisha ya baharini na kuzuia kupotea kwa matumaini yanayohamasisha watu kuhatarisha maisha yao kwa kuanzia.” Amesisisitiza Bwana Conchetel.

Vikosi vya UNHCR vimenawapatia manusura msaada wa matibabu na wa kibinadamu. Tukio hili limekuja wiki chache baada ya tukio linguine la kuzama kwa Meli ambapo maisha ya watu 150 yanakadiriwa kupotea katika tukio moja tu kwa mwaka huu katika bahari ya Mediterania.

Kufuatia janga la leo, inakadiriwa kuwa watu 900 tayari wamepoteza maisha wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kwa mwakahuu wa 2019.