Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tulipoteza watu wengi wakati wa vita; hatutaki kupoteza watu wengi zaidi-Susan Kiden UNMAS

Suzan Kiden Dominic, mteguaji mabomu aliyefundishwa na UNMAS
UNMAS
Suzan Kiden Dominic, mteguaji mabomu aliyefundishwa na UNMAS

Tulipoteza watu wengi wakati wa vita; hatutaki kupoteza watu wengi zaidi-Susan Kiden UNMAS

Amani na Usalama

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusiska na uelimishaji na uteguaji wa mabomu ya ardhini na vifaa vingine vya mlipuko UNMAS imeteketeza rundo la mabomu ya kutegwa ardhini yaliyogundulika kilomita 40 nje ya mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. 

Baada ya kupokea taarifa za uwepo wa mabomu hayo ya kutegwa ardhini, timu ya ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusiska na uelimishaji na uteguaji wa mabomu ya ardhini na vifaa vingine vya mlipuko UNMAS kwa haraka ikasafiri kuelekea eneo hilo la Kuruki ikiwa ni sehemu ya jitihada zake kuzisaidia jamii kurejea nyumbani na pia kuweka mazingira salama.

Mabaki ya silaha mbalimbali hususani mabomu ya kutegwa ardhini mara nyingi ni moja ya vyanzo vikubwa vya vifo katika maeneo yaliyokuwa na vita.

Kwa Sudan Kusini, hususani katika nyakati hizo ambazo ambazo wananchi wanarejea makwao na kujaribu kurejea katika maisha yao ya kila siku, ardhi ni moja ya sehemu za hatari.

Stephen Ladu, mkazi wa Kuruki ndiye aliyewataarifu maafisa wa UNMAS kuhusu vilipuzi hivyo, na anasema ana wasiwasi na ustawi wa watoto na wanawake katika eneo hilo.

(Sauti ya Stephene Ladu)

“Nilivikuta vitu hivi hapa na wanawake na watoto wamekuwa wakiteka maji kutoka eneo hili. Na msimu wa ukame unakaribia. Kwa hivyo, nilifikiri vitu hivi vitasababisha madhara na nikaamua kuwaonesha wategua mabomu.”

Baada ya kulitambua eneo lenye vilipuzi ambavyo vimesalia bila kulipuka, kikosi cha UNMAS kikaanza mchakato wa kuviharibu vilipuzi hivyo chini ya usimamizi wa George Murunda ambaye amekuwa akifanya kazi hii ya uteguaji wa mambomu kwa miaka 25 na hata amepoteza mkono wake wa kulia kutokana na kazi hii.

(Sauti ya George Murunda)

“Tuliwauliza wana Kijiji kama kuna athari yoyote ya mambomu ambayo hayajalipuka katika Kijiji na wakasema ndio. Na sasa kuanzia hapo, tukasema sawa mmesema ndio, yako wapi? Kisha wakaja hapa pamoja nasi wakatuonesha haya milimita 6 kwa milimita 106, yalikuwa hayajalipuliwa.”

Akiwa mwenye nguvu na shauku kuhusu kazi yake, Suzan Kiden alikuwa miongoni mwa wale waliochimba mashimo kwa ajili ya kuteketeza silaha hizo.

Akiamini kuwa kazi yake inaokoa maisha, anaeleza matumaini yake ya kuona nchi yake ikiwa bila mabomu ya kutegwa ardhini pamoja na silaha nyingine zilizoachwa bila kulipuka.

(Sauti ya Suzan Kiden)

“Ninafanya kazi kwa nguvu kwasababu ninataka kuokoa maisha ya watu wangu katika nchi yangu. Tulipoteza watu wengi wakati wa vita; hatutaki kupoteza watu wengi zaidi. Hayo mabaki ya vita ni adui hatari kwa maisha yetu.”