Skip to main content

Jamhuri ya Afrika ya Kati sasa ni ya 3 duniani kwa kuwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu

C.A.R  sasa ni ya 3 duniani kwa kuwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu. Mapema mwaka huu, UNICEF ilisema watoto zaidi ya 43,000 waliochini ya umri wa miaka mitano nchini humo huenda wakafariki ndani ya mwaka huu wa  2019 kutokana na utapiamlo uliokithiri
UNICEF/Ashley Gilbertson
C.A.R sasa ni ya 3 duniani kwa kuwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu. Mapema mwaka huu, UNICEF ilisema watoto zaidi ya 43,000 waliochini ya umri wa miaka mitano nchini humo huenda wakafariki ndani ya mwaka huu wa 2019 kutokana na utapiamlo uliokithiri

Jamhuri ya Afrika ya Kati sasa ni ya 3 duniani kwa kuwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu

Msaada wa Kibinadamu

Watu wawili kati ya watu watatu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wanahitaji msaada wa kibinadamu na hivyo kufanya janga hilo la kibinadamu kuwa la tatu kwa kubwa zaidi duniani baada ya Yemen na Syria, limesema shirika la mpango duniani la Umoja wa Mataifa, WFP

Takwimu hizo zinamaanisha kwamba takribani watu milioni 3 nchini humo Jamhuri ya Afrika ya kati, C.A.R wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Msemaji wa WFP Herve Verhoosel ambaye alikuwa ziarani nchini humo wiki hii ameshuhudia hali halisi ya janga hilo akisema kuwa hali nchini CAR imedorora zaidi kwa kipindi cha miezi 18 iliyopita, na hivyo kusababisha ongezeko la mahitaji ya kibinadamu.

(Sauti ya Herve Verhoosel)

“Ingawa kutia saini kwa makubaliano ya amani kati ya serikali na makundi 14 ya wapiganaji mnamo tarehe 6 Feburuari 2019 vimeboresha hali ya amani katika baadhi ya maeneo, hali ya kibinadamu bado ni tete. Utapiamlo sugu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano umebaki katika kiwango cha juu cha asilimia 38 nchini kote. Unyafuzi nao unasalia katika viwango vya juu, ikiwa ni takribani mtoto mmoja kati ya watoto 10   wa kati ya umri wa miaka miwili hadi  sita. Mchanganyiko huu wa utapiamlo sugu na unyafuzi  ni wa kutisha na unaendelea kuweka maendeleo ya watoto hatarini.”

WFP inalenga kuendelea na misaada hasa kwa watu wenye uhitaji mkubwa kama vile watoto wachanga, wanawake wajawazito na wale wanaonyoyesha.

Kwa maana hiyo juu ya rasilimali za WFP zilizopo kwa sasa, dola milioni 35.5 zinahitaji kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2019 ili kufikia malengo ya kuongeza usaidizi mara mbili nchini C.A.R kufikia Desemba 2020.

Hadi kufikia sasa, nchi nne za juu zinazochangia shughuli za WFP nchini C.A.R ni Marekani, Ujerumani, Canada, na Uswisi.