Kampuni zaendelea kuitikia wito wa UN wa kuondokana na plastiki

21 Agosti 2019

Shirika la chakula na kilimo duniani FAO limeonyesha mfano wa manufaa yanayoanza kupatikana kutokana na matumizi mbadala ya bidhaa za plastiki, ikiwemo vifungashio ambavyo hivi sasa kampuni zinatengeneza ili kupunguza matumii ya vifungashio vya plastiki vinavyochafua mazingira.

Shirika hilo la chakula na kilimo duniani, FAO, limeaandaa video inayoanza kwa kuoyesha mto uliojaa taka za plastiki zikiwemo chupa na vifungashio vya vyakula, taka ambazo hatimaye zinaishia baharini.

Kwa mujibu wa takwimu za FAO, kila mwaka tani milioni 8 za taka za plastiki zinatupwa kiholela maeneo mbalimbali na kugharimu dola bilioni 13 za  uchumi wa dunia.

Huchukua miaka 500 kwa plastiki za kawaida kuoza, na hata zikimeng’enyuka na kuwa chembechembe bado zinaingia kwenye mfumo wa chakula wa binadamu kupitia samaki.

Kwa kutambua hilo kampuni ya PaperFoam nchini Uholanzi ilichukua hatua ya kukabiliana na vifungashio vya plastiki ambavyo ni asilimia 37 ya taka zote za plastiki.

Kampuni hiyo hutumia mabaki ya taka za kilimo na nyuzinyuzi za mbao kutengeneza vifungashio na sasa imefungua viwanda zaidi Uholanzi, Marekani, China na Malaysia.

Mark Geerts ni Afisa mtendaji wa PaperForm na anasema, “malighafi ya karatasi hizi ni wanga na selulozi za nyuzinyuzi na tunazipata katika nchi husika hatuagizi kutoka nje. Ni vifungashio vitokanavyo na taka zinazooza. Na mada kuu kwenye kampuni yetu ni kudhibiti hewa ya ukaa, na vifungashio hivi vinatoa kiwango kidogo zaidi cha hewa ya ukaa. Na hii inasaidia sana kampuni ambazo zinataka kupunguza uchafuzi wa hewa.”
 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter