Vituo vya CBCC nchini Malawi vyapunguza visa vya Kipindupindu

21 Agosti 2019

Nchini Malawi, vituo vya kulea watoto vinavyosimamiwa na kuendeshwa na jamii, CBCC, vimekuwa chachu kubwa katika kuimarisha huduma za kujisafi na hivyo kudhibiti magonjwa kama vile kipindupindu. 

Watoto wakiimba na kucheza katika kituo cha chekechea cha malezi ya watoto wilayani Chitipa nchini Malawi. Kituo hiki kinapata ufadhili kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Malawi na kupitia hapa watoto wanakuja asubuhi na kurudi nyumbani jioni wakipatiwa chakula, elimu ya darasani nai le ya kujisafi.

Elimu ya kujisafi ni pamoja na hii ambapo mwalimu anaelimisha ni vipi watoto wanaweza kutumia vizuri choo cha shimo na kuepuka maambukizi ya magonjwa. Watoto watumie sabuni, maji na pia wafunike shimo la choo baada ya kutumia.

Na walipoulizwa swali na kujibu wakiwa wamepatia ni makofi..

Esther Kangeya ni mlezi katika kituo hiki ambaye anasema, “ni vyema watoto wakajifunza mapema tabia nzuri na tabia hizo husalia kwa mtoto kadri anavyokua. Wataendelea na tabia nzuri ya kunawa mikono kila wakati wanapotumia choo. Wazazi nao nyumbani wamejenga vyoo na kuweka huduma za kujisafi.

Na sasa jamii zimeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa vituo hivi ni endelevu kwa kutenga maeneo ya shule, wanafyatua matofali na UNICEF ikajitolea kujenga vyoo.

Wakazi wa Chitipa wamekubaliana kuwa vyoo vinasafishwa kila siku na kila wiki lazima wakutane kusafisha mazingira ya vituo ili watoto wajifunze vyema na wasipate magonjwa na tayari visa vya kipindupindu, ugonjwa ambao unaongoza kwa vifo vya watoto wenye umri wa chini  ya miaka 5 nchini Malawi vimepungua.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud