Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali si shwari Murzuq nchini Libya, pande kinzani lindeni raia- OCHA

Mji mkongwe wa Benghazi, Libya Februari 2019
UN OCHA/GILES CLARKE
Mji mkongwe wa Benghazi, Libya Februari 2019

Hali si shwari Murzuq nchini Libya, pande kinzani lindeni raia- OCHA

Amani na Usalama

Takribani raia 90 wameuawa na wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa tangu kuongezeka kwa uhasama kati ya pande kinzani kuanzia mwezi huu kwenye mji wa Muruzq ulioko kusini-magharibi nchini Libya. Ripoti zinaongeza kuwa katika kipindi hicho watu 9,450 wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo.

 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada ya dharura, OCHA imesema miongoni mwa waliofariki dunia ni watu 45 ambao waliuawa kwa kombora lililorushwa kutoka angani tarehe 4 mwezi huu wa Agosti na watoto wengine 6 ambao waliuawa au kujeruhiwa tarehe 8 mwezi huu baada ya kombora kutua kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani katika kitongoji cha Bendalwah.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa OCHA Jens Laerke amesema waathirika wako pande zote za mapigano kutokana na mashambulizi ya kiholela yanayofanywa kwa kutumia ndege, ndege zisizo na abiria pamoja na maroketi.

(Sauti ya Jens Laerke)

“Takribani watu 9, 450  sasa wamekimbia makazi yao kutokana na mashambulio hayo kwenye mji wa Murzuq tangu mwezi huu wa Agosti lakini baadhi ya familia zinahofia kukimbia maeneo yenye mapigano kwa sababu wanaogopa kulipiiwa kisasi. Iwapo familia itakimbia kutoka eneo linalodhibitiwa na pande moja kinzani, basi upande mwingine unaweza kufikiria kuwa wana uhusiano na adui, hivyo basi familia zinahofia kulengwa”

Bwana Laerke amesema mahitaji ya kibinadamu nayo yanaongezeka, ambapo kipaumbele zaidi hivi sasa ni huduma za afya, chakula, maji,  huduma za kujisafi halikadhalika blanketi.

Umoja wa Mataifa na mashirika ya kibinadamu wanachukua hatua kusambaza misaada hiyo lakini kuna vikwazo vya kuingia Murzuq kwa kuwa barabara zimeharibiwa na kuna vizuizi vingi njiani.

Hata hivyo msemaji huyo wa OCHA amesema kuwa kadri mahitaji ya kibinadamu yanavyozidi kuongezeka, wanatoa wito kwa pande hizo kinzani zihakikishe kuna mazingira salama kwa misaada kufikia wahitaji na wahakikishe raia wanaweza kuondoka pindi watataka kufanya hivyo.

Halikadhalika amekumbusha jamii ya wahisani kuongeza fedha zaidi ili kukidhi ombi la usaidizi wa kibinadamu kwa Libya ambapo kati ya dola milioni 202 zinazohitajika, hadi sasa wamepokea dola milioni 60 pekee, nusu ya fedha hizo zikiwa ni kutoka kamisheni ya Ulaya.